KCB yachukua uongozi wa mapema katika raga ya kitaifa
Na GEOFFREY ANENE
KLABU ya KCB inaongoza mashindano ya raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande baada ya kunyakua taji la duru ya ufunguzi ya Kakamega Sevens iliyoandaliwa Jumapili.
KCB, ambayo ilishinda makala hayo ya kwanza ya Kakamega Sevens kwa kucharaza mabingwa wa Kenya mwaka 2018 Homeboyz 21-12 katika fainali ya kusisimua, ina alama 22.
Mabingwa wa Kenya mwaka 2013 na 2014 KCB wako alama tatu mbele ya Homeboyz nao Mwamba, ambao wanajivunia kuwa na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya miguso mingi kwenye Raga ya Dunia Collins Injera katika kikosi chao, waliridhika na nafasi ya tatu kwa kubwaga wafalme wa mwaka 2015 Nakuru 24-0 katika mechi ya kuwania medali ya shaba.
Washindi wa mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 Mwamba wamezoa alama 17, mbili zaidi ya Nakuru.
Mabingwa wa mwaka 2009 Strathmore Leos wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 13 baada ya kunyamazisha miamba Nondies 21-19 katika fainali ya nambari tano na sita.
Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) na washindi wa mwaka 1999, 2000, 2001 na 2004 Impala Saracens waliopoteza katika nusu-fainali ya kutafuta nambari tano hadi nane, wana alama 10 kila mmoja.
Menengai Oilers inashikilia nafasi ya tisa kwa alama nane baada ya kushinda Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi 17-5 katika fainali ya kitengo cha Challenge Trophy. Machine inafunga 10-bora alama moja nyuma.
Egerton Wasps na wafalme wa mwaka 2017 Kabras Sugar wamezoa alama tano kila mmoja.
Wanapatikana katika nafasi ya 11 na 12, mtawalia.
Majirani
Majirani wa Kabras, Western Bulls waliambulia alama tatu na kumaliza duru ya ufunguzi katika nafasi ya 13.
Kisii ilichapwa 17-12 na Bulls katika fainali ya kutafuta nambari 13. Ilikamilisha kampeni yake ya Kakamega katika nafasi ya 14 kwa alama mbili.
Kisumu, ambayo pamoja na Bulls zimerejea katika Ligi Kuu, ilipata alama moja sawa na washindi wa mwaka 2005, 2006 na 2012 Kenya Harlequin waliosikitisha katika nafasi ya mwisho.
Duru ya pili ni Kabeberi Sevens mnamo Julai 27-28 uwanjani Kinoru, kaunti ya Meru. Mji wa Kisumu utaandaa duru ya tatu ya Dala Sevens mnamo Agosti 10-11 uwanjani Mamboleo Showground.
Duru ya nne itakuwa ya Prinsloo Sevens mjini Nakuru mnamo Agosti 17-18. Christie Sevens itafanyika Agosti 31 hadi Septemba 1 uwanjani RFUEA, huku Driftwoods ikifunga mashindano haya mnamo Septemba 7-8 mjini Mombasa.
Mashindano haya ya kitaifa yatatumika na Shirikisho la Raga Nchini (KRU) kutafuta wachezaji wa timu ya Shujaa watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Kombe la Afrika baadaye mwaka huu pamoja na Raga ya Dunia ya msimu 2019-2020.