HabariKimataifaSiasa

Kenya yarejeshea TZ dhahabu ya Sh100m

July 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

PETER MBURU na MARY WANGARI

[email protected]

KENYA Jumatano ilirejesha kilo 35 za dhahabu ambayo ilinaswa humu nchini na polisi hadi Tanzania, wakati mataifa hayo yanashirikiana kukabiliana na biashara haramu.

Kundi la maafisa wa serikali kutoka Nairobi wakiongoza na Waziri wa Masuala ya Nje Monica Juma na Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji walifika Tanzania kurejesha dhahabu hiyo, ambayo ilikamatiwa jijini Nairobi.

Bado haijafahamika dhamani halisi ya dhahabu hiyo, lakini inakisiwa kuwa ya Sh100 milioni.

Dhahabu yenyewe ilipokelewa na Rais John Pombe Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam, ikikaguliwa mbele ya umma kubaini kuwa ni dhahabu ya kweli.

Wakati hafla hiyo ikiendelea, Rais Uhuru Kenyatta alipiga simu kutoka Nairobi kueleza nia ya Kenya kushirikiana na Tanzania, hatua ambayo imetekelezwa siku chache tu baada ya Rais Kenyatta kumtembelea Rais Magufuli Tanzania, ambapo walifanya mazungumzo.

Mazungumzo yalilenga kutatua tofauti za kibiashara ambazo zimekuwapo baina ya Kenya na Tanzania, na Rais Magufuli alieleza kuwa Kenya imeeleza nia ya kununua unga kutoka Tanzania, pamoja na gesi.

Alipopiga simu, Rais Kenyatta alimwambia Magufuli “Ndugu yangu nasema tutaendelea kufanya kazi pamoja kwani Kenya na Tanzania hazina mipaka jinsi tulielewana. Tusaidiane kumaliza ufisadi na kurejesha pesa ambazo zimeibiwa kutoka kwa watu wetu ili tulete maendeleo.”

Mawasiliano yao yalisheheni utani lakini yakadumisha ajenda yao kuu ya kuwasaidia wananchi.

“..endelea wanakushangilia watu hapa kwa maneno mazuri uliyozungumza. Hebu mmshangilieni tena mheshimiwa Uhuru,” alisema Rais Magufuli.

“Tumesema kwamba tunataka kuhakikisha kwamba yale ambayo wananchi wametupatia imani yao, kutupatia uongozi sisi yetu ni kuhakikisha kwmaba tumetenda haki na tumelinda mali ya wananchi wetu na mali hiyo iende kutujengea barabara, hospitali, shule.. Walaghai hawana nafasi katika nchi zetu tena.

Rais Magufuli kwa upande wake alimshukuru Bw Kenyatta akisisitiza kwamba uhusiano wa Kenya na Tanzania uko imara na kamwe mataifa haya mawili hayatatenganishwa.

“Mheshimiwa Rais nakushukuru sana kwa maneno mazuri. Undugu wa Kenya na Tanzania uko pale pale kamwe hapatatokea mtu wa kututenganisha. Tutaendelea kupendana mpaka maendeleo ya Wakenya na Watanzania yaweze kupatikana.”

“Ninawaambia Rais Uhuru ana moyo wa kizalendo. Anawapenda Wakenya na ana wapenda Watanzania, Niliwaambia ningekuwa mbaya tungezungumza kisirisiri hizi hela hawangeziona Watanzania. Tungetaka tungegawana polepole. Wangebaki kuandika kwenye magazeti lakini hela zimeliwa,” alisema Rais Magufuli akisisitiza kwamba ni hatua hiyo ilitokana na upendo wao kwa wananchi,

Kenya imekuwa ikijikaza kukabili biashara haramu ya dhahabu kutoka eneo hili hasa nchini DR Congo, kwani uwanja wa ndege wa kimataifa JKIA ulikuwa umefanywa mahali pa kupitishia madini hayo.