Makala

AKILIMALI: Maembe yana mapato kwa wanaokuza miche iliyoimarishwa

July 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KWA zaidi ya miaka 20, Mary Njuguna amekuwa akivuna maembe kutoka kwenye miembe miwili.

Yeye hufanya kilimo-mseto eneo la Thunguri, Kaunti ya Kirinyaga ambapo pia ana miparachichi.

Hata ingawa hana takwimu za kiwango cha maembe anayovuna, Mary anasema anayazalisha katika miembe aliyoipanda kupitia mbegu.

Kulingana na wataalamu wa kilimo maembe yanayopandwa kupitia mkondo huo huchukua kati ya miaka 7-15 kuanza kuzalisha.

Mkulima Mary hata hivyo anasema mazao anayopata ni salama, kwani hayajakuzwa kwa kemikali kama vile kupulizia dawa dhidi ya magonjwa au wadudu.

“Miti yenyewe niliipanda kwa mbolea ya mifugo, na sijawahi kuipulizia dawa yoyote,” anasema.

Mfumo wake wa kilimo ni hai, ambapo hutumia mbinu asili kukabili changamoto za wadudu na magonjwa.

Aidha, anasema maembe ya kutoka katika shamba lake ni matamu.

Matunda anayovuna ni madogo hivyo embe kijumla hununuliwa kati ya Sh2-3.

“Mengine huozea shambani kwa sababu ya bei duni,” analalamika.

Uimarishaji

Wataalamu wa kilimo wanasema ili kupata mazao bora ya maembe mkulima hana budi kukumbatia miche iliyoimarishwa.

Bw Daniel Mwenda wa Mwenda D Agroforestry Solution anaeleza kwamba matunda yanayozalisha vyema ni yale yaliyopandwa kutoka kwa miche ya kupandikiza (grafted).

“Miche ya kupandikiza imetafitiwa Kisayansi na kubainika kuzalisha matunda bora-makubwa na mengi,” anasema Bw Mwenda.

Anabainisha kwamba miembe ya kupandikizwa huchukua kati ya miaka mitatu hadi mitano kuanza kuzalisha.

Kwa maelezo yake, basi mkulima kama Mary anapaswa kupanda miche yake ili kuepuka vikwazo vya soko.

Kulingana na mtaalamu huyu miembe iliyotunzwa ifaavyo, kwa msimu mmoja huzalisha wastani wa matunda 200.

Msimu mmoja ni sawa na mwaka mmoja.

Aghalabu maembe mengi nchini huvunwa kipindi cha kati ya Novemba-Machi.

Agnes Omingo ni mkuzaji wa miembe iliyopandikizwa katika Kaunti ya Kajiado na anasema kando na kuchukua muda mfupi kukomaa na kuanza kutunda, maembe hayana kikwazo cha soko.

Bi Agnes Omingo ni mkuzaji wa miembe iliyopandikizwa katika Kaunti ya Kajiado. Picha/ Sammy Waweru

Kwa mujibu wa maelezo ya mkulima huyu ni kwamba maembe ni miongoni mwa mimea na matunda rahisi mno kupanda.

Aidha, baada ya shamba kuandaliwa miche inapandwa kwa kipimo cha mashimo futi 30 kwa 30 mraba.

“Matunda haya yanahitaji udongo usiotuamisha maji na wenye kiwango cha asidi, pH, 4.5-7.0,” anasema mtaalamu Daniel Mwenda.

Urefu wa mashimo yake kuenda chini yanapaswa kuwa sentimita 60 na upana wa kipimo sawa na hicho.

Agnes naye anasaidia kutoa maelezo ya utaratibu mzuri wa kilimo kwa ajili ya kuzalisha maembe.

“Udongo uchanganywe na mbolea ya mifugo sawasawa. Mchanganyiko huo uwekwe shimoni kimo cha karibu sentimita 30,” anaeleza Agnes.

Anafafanua kwamba mkulima amwage maji kwenye shimo lile halafu aandae shimo dogo kupanda mche.

Kimo kilichosalia, sentimita 30 ni cha kutunza mimea ile kwa mbolea na maji.

“Maji na mbolea ni viungo muhimu katika kilimo cha matunda,” anasisitiza Agnes.

Mama huyu pia hukuza mapapai, machungwa na zabibu.

Changamoto kuu kwa maembe ni mdudu aina ya Fruit fly.

Ni mdudu haribifu anayetoboa matunda, na kuyaacha yakioza. Ili kudhibiti magonjwa na wadudu kwa matunda, mkulima anahimizwa kushirikisha mtaalamu au wataalamu wa kilimo ili kupata ushauri wa njia na dawa bora kutumia.

Maembe ya miche ya kupandikizwa yana uzito, ambapo yale makubwa moja lina uwezo wa kuwa na zaidi ya kilo moja. Bei yake ni ya kuridhisha, Agnes akifichua kwamba huuzia wateja wake zaidi ya Sh10 kila tunda.