Habari MsetoSiasa

Kichapo kwa wanasiasa fisadi

July 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

 BRIAN WASUNA na BENSON MATHEKA 

WATUMISHI wa umma wenye maazimio ya kisiasa walioshtakiwa kwa ufisadi, na wanasiasa wanaokumbwa na kesi za ufisadi wamepata pigo kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba, maafisa wanaoshtakiwa kwa ufisadi hawafai kukanyaga afisi zao kabla ya kesi kuamuliwa.

Wanaharakati wanasema kwamba, kufuatia uamuzi huo, Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) haina budi kuwazuia wanaokabiliwa na kesi kugombea viti tofauti kwenye uchaguzi.

Mnamo Jumatano, Jaji Mumbi Ngugi aliamua kwamba kuruhusiwa kwa washukiwa kurejea katika ofisi zao wakishtakiwa kwa ufisadi, ni kukiuka kifungu cha sita cha katiba kuhusu maadili ya maafisa wa umma na kinyume cha misingi ya utawala bora na uongozi.

Jaji Mumbi alikuwa akitoa uamuzi katika kesi ambayo Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal Kassaine alitaka mahakama ibatilishe uamuzi wa mahakama ya ufisadi iliyomzuia kukanyaga katika ofisi yake bila idhini ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi.

Hatua hii itazuia maafisa wakuu wa serikali wakiwemo wabunge, magavana, mawaziri, makatibu wa wizara, makamishna wa tume za kikatiba na wakurugenzi wa mashirika ya umma kurejea kazini wakishtakiwa kwa ufisadi na kutumia vibaya mamlaka yao.

Jana, wanaharakati walipongeza uamuzi wa Jaji Mumbi ambao ulijiri siku moja baada ya waziri wa fedha Henry Rotich na katibu wa wizara hiyo Kamau Thugge kusimamishwa kazi waliposhtakiwa kwa ufisadi.

Katika uamuzi wake, Jaji Mumbi alisema sehemu ya 62(6) ya sheria ya kupambana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi ambayo washukiwa walikuwa wakitumia kurejea kazini ni kinyume cha katiba.Sehemu hii inasema maafisa wa umma ambao vipindi vyao vimewekwa kikatiba na kuna utaratibu wa kuwaondoa mamlakani hawawezi kusimamishwa kazi wakishtakiwa.

Kulingana na Kituo cha Kimataifa kuhusu Sera na Mitafaruku (ICPC), uamuzi huo ni pigo kwa maafisa wa umma wanaotumia sehemu za sheria ya ufisadi kusalia afisini wakishtakiwa kortini. Kulingana na shirika hilo, sehemu hii ya sheria ilikuwa ikiendeleza ufisadi na kufanya wanaoutekeleza kuepuka adhabu hasa wale waliochaguliwa.

Kwenye taarifa, ICPC ililaumu tume hiyo kwa kuchangia ufisadi serikalini kwa kuruhusu watu ambao maadili yao yanatiliwa shaka kugombea viti kwenye uchaguzi.

“IEBC haina budi kuweka sheria kali kuekeleza vyama vya kisiasa kuchapisha majina ya wawaniaji na kesi zao zinazoendelea kortini. Hii itakuwa hatua muhimu ya kutakasa siasa za Kenya na viongozi wanaokabiliwa na makosa mabaya wanaoingiza uhalifu katika siasa.

“Kuzuia kuingiza uhalifu katika siasa Kenya hakuwezekani kwa kupiga marufuku wabunge walio na rekodi ya uhalifu lakini unapaswa kuanza kwa kutakasa vyama vya kisiasa,” ilisema taarifa ya ICPC.

Shirika hilo linasema IEBC inafaa kuwahakikisha wawaniaji wanafichua rekodi yao ya uhalifu katika hati ya kiapo kisha rekodi hiyo itangaziwe umma.