MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ni muhimu kuwa na subira kwa mitihani unayotahiniwa na Allah
Na HAWA ALI
SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla.
Swala na salamu zimwendee kipenzi wa ummah huu, Mtume wetu Muhammad, Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.
Ndugu yangu katika imani-Allah Taala atupe imani ya kweli itakayotupa kheri za duniani na akhera-Aamiyn!
Tunaendelea kuusiana katika mapenzi ya Allah, ufahamu na uelewe kwamba miongoni mwa mambo makubwa yenye kuokoa ni kusubiri kwa mitihani unayotahiniwa na Allah.
Subira yako hii iende sambamba na kuzishukuru neema za Allah alizokuneemesha na kuipa mgongo dunia imshughulishayo mja kiasi cha kumsahau Allah Mola Muumba wake.
Elewa kuwa subira ni miongoni mwa ibada ngumu lakini zenye fadhila kubwa kabisa. Subira ni hitajio muhimu la kila muumini katika hali zake zote na katika kipindi chake chote cha kuishi katika ardhi hii ya Maulana.
Subira ni siri na ufunguo wa fanaka, furaha, amani, salama na mafanikio yote katika ulimwengu huu wa mpito na ule wa milele.
Qur-ani Tukufu imesheheni aya kathiri zinazotaja fadhila za subira, aya hizi zinashereheshwa na hadithi adida (nyingi) za Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Hebu tuzitafakari kwa pamoja aya zifuatazo tuone namna gani Allah anavyotuita katika biashara ya subira; biashara isiyododa wala kukhasirika, tusome:
“Enyi mlioamini! jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na swala; bila shaka allah yu pamoja na wanaosubiri” [2:153]
Haya mpenzi ndugu yangu-Allah atupe fahamu-tunaelewa nini katika aya hii tukufu? Bila shaka utakubaliana nami ndugu yako kuwa aya hii inaeleza kuwa muumini ndiye mlengwa na shabaha ya mitihani na misukosuko kama inavyotuwazikia kupitia aya hii:
“Na tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); khofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. na wapashe khabari njema wanaosubiri”. [2:155]
Tayari imetuthibitikia kuwa muumini ni lazima ataonjwa na Mola wake kwa kumtahini kwa mitihani mbalimbali, hana pa kukimbilia.
Sasa la msingi la kujiuliza ni je, akisibiwa na masaibu na mitihani hii ya Mola wake afanye nini? Aya ikatoa dawa na kuonyesha kuwa tegemeo na kimbilio pekee la muumini wakati wa masaibu na misukosuko ni SUBIRA na SWALA.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema subira na swala ni silaha kali inayompa ushindi mnono muumini katika vita vigumu va masaibu na misukosuko ya maisha ya kila siku.
Aya ikamalizia kwa kueleza daraja na cheo cha wanaosubiri na kuswali pindi waonjwapo na Mola wao kuwa watakuwa pamoja na Allah.
Yaani msaada wa Allah utakuwa pamoja nao katika dhiki na masaibu yote ya leo hapa duniani na ya kesho kule akhera.
Mpenzi ndugu yangu, je unapenda kupendwa na Allah? Kama unapenda na bila shaka hakuna asiyependa, basi subiri unaposibiwa na masaibu yatokayo kwa Allah, kwani subira hiyo ndio thamani ya kuyanunulia mapenzi ya Allah, tusome pamoja na tuamini: “…na Allah anawapenda wafanyao subira”. [3:146]
Ndugu yangu-Allah atuwafikishe kusubiri-tuendelee kutafakari pamoja kwa maslahi na manufaa ya nafsi zetu wenyewe. Allah Mola Mwenyezi anamkhutubu Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-kwa kumwambia: “na subiri na kusubiri kwako kusiwe ila kwa ajili ya Allah tu…” [16:127]
Sote tunatambua kuwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipewa na Mola wake jukumu gumu na zito la kuufikisha ujumbe wake kwa waja wake.
Misukosuko
Katika kulitekeleza jukumu hili Bwana Mtume alikumbwa na misukosuko mikubwa ambayo ilikuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikisha ujumbe wa Allah kwa waja wa Allah.
Ndipo Allah aliyemtuma mja wake kwa waja wake akamuagiza Mtume wake kusubiri. Kwa kuwa kusubiri tu hakutoshi anamwambia subira yake yote iwe ni kwa ajili yake yeye tu Allah ambaye ndiye atakayewalipa wote wanaosubiri: “…na bila shaka wafanyao subira (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya ya twaa) watapewa ujira wao pasipo hesabu”. [39:10]
Bwana Mtume akanyenyekea na akajisalimisha kwa Mola wake, akasubiri kwa ajili ya Allah mpaka nusura ya Allah na ushindi ukapatikana na watu wakaingia katika dini ya Allah makundi kwa makundi.
Nasi basi ewe ndugu yangu katika Uislamu tumuige na kumgeza Mtume wa Allah katika kusubiri kwa ajili ya Allah ili itufikie nusra na ushindi kutoka kwa Allah.
Ewe ndugu yangu, nakusihi tukiri kuwa muumini ana haja kubwa kuelekea subira wakati wa kufikwa na mabalaa mbalimbali yasiyo na hodi wala taarifa.