Habari

MAJONZI KWA SHUJAA: Mbunge Okoth aombolezwa

July 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUZUNI kuu ilitanda Ijumaa katika eneobunge la Kibra, na taifa kwa jumla, kufuatia kifo cha Mbunge Ken Okoth aliyefariki baada ya kuugua saratani ya utumbo.

Okoth aliyekuwa na umri wa miaka 41 alikuwa akihudumu kwa muhula wa pili.

Alifariki katika Hospitali ya Nairobi alikolazwa Alhamisi usiku baada ya hali yake ya afya kudhoofika.

Alikuwa amerejea nchini mapema Julai kutoka jijini Paris, Ufaransa ambako alikuwa akipokea matibabu kwa muda wa miezi mitano iliyopita.

Kifo chake kinajiri chini ya mwezi mmoja tangu ugonjwa huo huo wa kansa umuue aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano ya Safaricom, Bob Colymore.

Marehemu Collymore alifariki Julai 1, 2019, baada ya kuugua kansa ya damu kwa muda wa zaidi ya miezi minane.

Kulingana na Imra Okoth, ambaye ni meneja wa afisi ya eneobunge la Kibra, marehemu Okoth alifariki baada ya kuomba mitambo ya kumsaidia kupumua izimwe.

“Mheshimiwa aliletwa katika Hospitali ya Nairobi saa kumi na moja jioni. Hali yake ilipoendelea kuwa mbaya alihamishwa hadi katika kitengo cha wagonjwa mahututi ambako alifariki baada ya saa moja iliyopita,” Bw Okoth akawaambia wanahabari nje ya hospitali hiyo.

Marehemu Okoth aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mnamo 2013 baada ya eneo bunge la Kibra kugawanywa kutoka kwa eneobunge la Langata.

Eneo hilo zamani lilikuwa likiwakilishwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga tangu 1992.

Bw Okoth alishinda kiti hicho kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya chama cha ODM baada ya kuwashinda wapinzani wa vyama vingine ikiwemo Jubilee.

Kabla ya kuingia katika ulingo wa siasa, marehemu alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Children of Kibra ambalo lilifadhili miradi mbalimbali ya kuwasaidia wakazi wa vitongoji duni katika eneo bunge hilo.

Bw Okoth alisomea nchini Amerika ambako aliwahi kufanya kazi kama mwalimu wa shule ya upili kati ya miaka ya 2005 na 2009. Marehemu atakumbukwa kama kiongozi kijana na mchapa kazi aliyehusudi miradi inayofungamana na elimu.

Hadi kifo chake, alikuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu elimu inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly.

Rais Uhuru Kenyatta Naibu wake William Ruto na Bw Odinga waliwaongoza viongozi wengine kutuma salamu za pole kwa familia, marafiki na wakazi wa eneobunge la Kibra.

Rais alimtaja Okoth kama kiongozi jasiri na shupavu aliyejitolea kuwahudumia watu wa Kibra na taifa kwa jumla kwa moyo wa kujitolea.

“Nimepokea habari za kifo cha Mbunge wa Kibra Mheshimwa Ken Okoth kwa huzuni mkubwa. Mungu aifariji familia, marafiki, jamaa, wakazi wa eneo bunge lake na Wakenya kwa jumla wakati huu mgumu wa maombolezo,” Rais Kenyatta akasema.

Naye Bw Odinga akasema: “Nimehuzunishwa mno na kifo cha Mbunge wetu Mheshimwa Ken Okoth. Ken alipambana na kansa kijasiri akiwahudumia wakazi wa eneo bunge hadi dakika za mwisho maishani mwake. Mungu aipe familia yake nguvu kustahimili msiba huu.”

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alimtaja marehemu kama kiongozi mwenye maono na aliyechukulia majukumu yake bungeni kwa makini.