• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
SHERIA: Utaratibu wa kisheria wa ndoa ya kitamaduni

SHERIA: Utaratibu wa kisheria wa ndoa ya kitamaduni

Na BENSON MATHEKA

NDOA ya kitamaduni kama aliyofunga Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru inatambuliwa katika sheria ya ndoa ya Kenya na inafaa kusajiliwa rasmi miezi mitatu baada ya sherehe zote za kitamaduni kukamilika.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa ndoa inayotambuliwa ni inayofungwa kwa kutumia desturi za jamii za humu nchini pekee.

Hii inamaanisha kuwa iwapo mwanamke Mkenya anaolewa au mwanamume Mkenya kuoa mtu wa jamii ya kigeni kupitia ndoa ya kitamaduni, ni lazima watumie desturi za jamii ya mchumba anayetoka nchini.

Sheria ya ndoa ya Kenya inasema kwamba ndoa ya kitamaduni haiwezi kusajiliwa ikiwa mahari haijalipwa hasa ikiwa desturi za jamii ya Bi Harusi inasema ilipwe.

Sheria inasisitiza kuwa mahari inapotakiwa kulipwa, inachukuliwa kuwa thibitisho la ndoa ya kitamaduni.

Ni baada ya kukamilisha sherehe zote na wanandoa kuanza kuishi pamoja ambapo ombi la kusajili ndoa ya kitamaduni linapaswa kuwasilishwa.

Kama nilivyotangulia kusema, linafaa kuwasilishwa ndani ya miezi mitatu. Ombi hilo ni sharti litaje wanandoa walitumia desturi za jamii gani kufunga ndoa yao na waape kupitia maandishi kwamba mahitaji yote ya jamii hiyo ya kuandaa ndoa yalifuatwa na kutimizwa kikamilifu.

Kiapo hicho kitakuwa na sahihi mbili za watu wazima ambao lazima wawe walitekeleza wajibu muhimu wakati wa sherehe za ndoa ya kitamaduni.

Kigezo cha umri ni muhimu

Ni lazima wanandoa wathibitishe kwamba walikuwa wametimiza umri wa miaka 18 wakati wa kuoana.

Hii inazuia watu kutumia desturi za jamii zao kushiriki ndoa za mapema.

Aidha, ni lazima ithibitishwe kuwa wanaofunga ndoa za kitamaduni hawana uhusiano wa kifamilia, kidamu au kuwa katika makundi ya watu ambao sheria hairuhusu waoane.

Ili kuhakikisha sheria imefuatwa kikamilifu, ni lazima ithibitishwe kuwa wanaofunga ndoa ya kitamaduni waliamua kufanya hivyo kwa hiari yao na wala hakuna aliyeshurutishwa.

Sheria inasema kwamba ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke walio na umri wa miaka 18 na zaidi.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Atumia taji la urembo kuboresha jamii yake

UMBEA: Usikurupukie ndoa sababu ya presha ya umri au jamii

adminleo