MWANAMUME KAMILI: Mke na mume ndio wajua dawa ya jipu liwashalo!
Na DKT CHARLES OBENE
TUNAPENDA sana kuitwa nyumbani kwa wengine kama wapatanishi!
Hili nalisema kwa ufasaha mno.
Wanaume kwa wanawake wanaona heri kuleta amani kwa majirani lakini kwao ni mahasidi wanaopigana kucha kutwa! Wanaona faraja kusuluhisha ya wengine ila yao nyumbani.
Vipi ikawa rahisi waja wa leo kupatanisha majirani ilhali wanaendeleza vita vyao vya nyumbani na kuzoa fedheha kwenye mitandao ya kijamii?
Hebu tegeni sikio niwajuze hekima ya maisha.
Mambo ya nyumbani sharti yatatuliwe nyumbani na watu wanaojua asili ya vita hivyo.
Mke na mume ndio tu wanaojua dawa ya jipu liwashalo.
Hakuna rafiki wala mshauri anayeweza kutatua vurugu asizoelewa asili wala fasili.
Hivyo basi, washauri hawana jukumu wala uwezo wa kupatanisha wanandoa walioamua wenyewe kupapurana badala ya kupendana!
Mwanamume kamili hukabili ndovu kwa mkonga wake!
Tatizo kubwa linalosibu nyumba zetu ni tabia za baadhi ya wanandoa kumwaga mtama kwenye kuku wengi! Hii tabia ya kuwaita wandani na masahibu kuja kupatanisha katu haizai suluhu.
Hakuna kuku asiyependa mtama wa bwerere. Nao kuku wa leo ndio kwanza wanafanya kila jitihada kuvuruga amani katika nyumba za masahibu kwa faida yao.
Watakuja kama wapatanishi lakini kusudi hasa ni kujipenyeza kuvuna kutoka nyoyo zinazolumba!
Kwa msingi, binadamu wakosanao ndio wapatanao!
Nyie wawili mnaokula vyenu kwa pamoja, mnaolala pamoja, tena mnaoishi na kufaana kwa umoja, ndio pekee wenye uwezo kusitisha ujuha na ununu na kuja pamoja kwa manufaa ya familia.
Washauri hawana kazi kujifanya wafariji huku wakipekua na kupakua mumo humo! Tahadharini nyie mnaopenda kuita jamaa na marafiki kuja “kusikiza na kusuluhisha!”
Kisa cha mume mmoja kuzaa na mwandani tena mshauri wa mkewe kimetufunza kwamba kuta za heshima zina nyufa nazo nguvu za mahaba hazina pazia. Si mara ya kwanza sisi kusikia kwamba mwinyi amepalilia kitongoji na sebule vilevile.
Isitoshe, akina baba nao wametimuliwa kwapani kwa wajakazi!
Katika hii dunia ambapo kina mama ndio kwanza wanaonja faida ya uhuru na kuwaachia wajakazi malezi nyumbani, vita vimenoga na baadhi ya kina mama wamejutia kuwaachia kuku mtama! Ukarimu wa mwanamume wa leo hauna mipaka.
Haja gani kuwaita watu wa nje kuja kuwapatanisha ilhali mmekwisha kuyavulia nguo na kukoga kwenye vidimbwi vyenu? Hakuna siri baina yenu. Hakuna jazba, watu kuwehuka ambazo kuta hazijashuhudia.
Isitoshe, kununiana siyo mwisho wa mahaba baina yenu. Mbona kuchukizana na kuhujumiana kama mahasidi? Hivi ndivyo visa vya leo vinavyochukiza maishani mwa wanawake kwa wanaume. Vita mnapigana lakini watoto wanazidi kuzaliwa baina yenu? Unafiki ulioje?
Kutofautiana baina ya mke na mumewe au baina ya wapendanao si tukizi maishani. Haya ni mambo yanayotokea kila mara na ambayo sharti tuyajulie kwa mapana.
Hata hivyo, kuna vijimambo vya aibu vinavyochusha maisha ya wangwana binadamu wa leo.
Si ajabu siku hizi kumwona mwanamume amenuna; hasemi hasemezeki ndani ya nyumba.
Aliyetumainiwa kama kichwa cha nyumba anakuwa mwingi wa hamaki, mkizi hasa.
Anasusia chakula cha mke. Hakogi nyumbani.
Hanunui kitu wala hatoi mchango wowote kwa manufaa ya familia yake. Kisa na maana? Ametofautiana na mkewe!
La ajabu zaidi ni kwamba mwanamume mnunaji hubadili si ngozi si sura akawa mnenaji – mwingi wa hadithi punde tu anapofika nyumba ndogo au kwenye kuta za mashangingi sisemi marafiki au washauri.
Ndio wanaume hao! Anaweza kususia kila kitu nyumbani kwake lakini hana aibu kula na kunywa na marafiki kwenye mikahawa.
Vilevile si nadra wanawake wa leo kutunga fundo la hamaki moyoni asimwajibikie mumewe kwa miezi kadha. Wanawake wa leo ndio wajuvi wa migomo ya kitoto ndani ya nyumba.
Hapiki hapikiki! Ndio wao hao wenye tabia za kuwaachia wanaume kujishughulisha upeo wa shughuli zao; wenyewe wakiwa usingizini ndoto kuziota.
Jamani wanadamu, hakuna kubwa lisilobebeka begani mwa wawili wanaojithamini na ambao wanapendana kwa dhati!
Ole nyinyi mnaotuzinga kwa yenu mili iliyojaa hadaa.
Mwili si kitu ikiwa huna akili kunyenyekea wema na kudumisha muamana! Vituko hivi tunavyoviona maishani ni ithibati ya jinsi binadamu walivyopungukiwa hekima na akili.
Jukumu la watu wazima ni kutambua thamani ya uhusiano, hadhi ya familia na kujua vipi kusuluhisha vijimambo vya nyumba pasipo kadhia za kutamkiana makuu au hata kununiana sebuleni na chumbani.
Waja kupatana hutegemea pakubwa uthabiti na ukomavu wa akili na hekima zao.
Kufuata upepo wa mapenzi au kusukumwa na jazba za ujanani pasipo mtu kukomaa akili huchangia kuwepo wanandoa au wapendanao wanaochukiza kwa zao tabia za kitoto na fedheha za mitandaoni. Hata ya nyumbani sharti kuyaitia majirani eti!
Mwanamume kamili hukabili ndovu kwa mkonga wake.
Hujizatiti kutatua ya kwake kabla kwenda kwa majirani.