• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
MWANASIASA NGANGARI: Maisha ya waziri Towett yalivyojaa vituko na ucheshi

MWANASIASA NGANGARI: Maisha ya waziri Towett yalivyojaa vituko na ucheshi

Na KENYA YEAR BOOK

DKT Taaitta Kipyegon arap Toweet alizaliwa mnamo 1925.

Alianzia masomo yake katika shule ya msingi ya Litein, kisha baadaye akajiunga na shule ya kimishenari ya Kabianga.

Katika mtihani wa kitaifa mnamo 1948, aliibuka mwanafunzi bora zaidi nchini na baadaye akajiunga na shule ya upili ya Alliance, kisha baada ya hapo akajiunga na chuo Kikuu cha Makerere.

Baada ya kukamilisha masomo katika chuo hicho aliendeleza masomo katika chuo kikuu kimoja Afrika Kusini, ambapo alipata shahada ya Filosofia.

Aliendelea na masomo na akapata shahada ya Uzamili katika Filosofia katika Chuo kikuu cha Nairobi, na baadaye shahada ya Uzamifu katika chuo hicho.

Towett alijitosa katika siasa 1958 alipochaguliwa kuwa mbunge Legco, kuwakilisha Kericho.

Wakati chama cha KADU kilipoanzishwa mnamo 1960, aliteuliwa kuwa mshauri wake mkuu wa kwanza, ambapo alianza kwa kutabiri kifo cha KANU ndani ya miezi minne. Alikuwa mmoja wa Wakenya mashuhuri ambao waliandika katiba katika kongamano la Lancaster, akiwakilisha KADU.

Vilevile, wakati KADU ilivunjwa na kumezwa na KANU 1964, ni Toweett peke yake ambaye alikataa kumezwa pamoja na wenzake wa chama hicho, akiamua kurejea debeni tena, lakini akabwagwa uchaguzini na kusahaulika kwa miaka mitano, ambapo alirejea.

Baada ya kushinda uchaguzi wa 1969, Rais Kenyatta alimteua kuwa Waziri wa Elimu. Katika uchaguzi uliofuata 1974, alichaguliwa tena lakini akapoteza uchaguzi wa 1979. Alikaa nje ya bunge hadi 1992 wakati aliteuliwa na KANU kuwa mbunge maalum.

Vilevile, aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kampuni ya Kenya Seed. Toweet pamoja na Jean Marie Seroney ambaye alikuwa mbunge wa Tinderet, Nandi ndio walikuwa wakipinga zoezi la jamii zingine kupewa mashamba eneo la Bonde la Ufa, ambayo jamii ya Kalenjin iliyaona kuwa yao tangu zamani.

Wawili hao walikuwa wakifanya mikutano ya umma kupinga zoezi hilo na alikubali tu baada ya Rais Mustaafu Daniel Moi kuunga zoezi hilo mkono.

Changamoto za Towett kisiasa zilianza miaka ya ’70 wakati kundi la wanasiasa lilijaribu kubadilisha katiba kumzuia Daniel Moi ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, kutokwea kuwa Rais endapo Rais Kenyatta angekufa.

Ilisemekana kuwa Toweett alionekana kuunga kundi hilo mkono, jambo ambalo lilizua tofauti baina yake na Moi, haswa ikizingatiwa kuwa moi baadaye 1978 aliingia katika Urais.

Towett alipoteza kiti chake cha ubunge kwa Profesa Jonathan Ng’eno katika uchaguzi huo. Mnamo 1988, alijaribu kujirejesha tena lakini akajiondoa mbioni akisema kuwa siasa zilikuwa chafu.

Awali miaka ya ’90 wakati nchi ilikuwa ikipigania kuwapo kwa vyama vingi, alikuwa akipigania kutokuwapo kwa chama chochote. Hata hivyo, aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa shirika la habari la Kenya Times Trust, ambalo lilikuwa likimilikiwa na KANU na ambalo liliandikia habari za kumsifia Rais Moi.

Kabla ya 2007, Towett alitahadharisha jamii ya Kipsigis kutojiingiza katika vyama vipya vya kisiasa, akisema vingewazuia kuwa katika serikali ambayo ingeundwa. Aliitaka jamii kujipima ikiwa ingenufaika kwa kujiunga na vyama hivyo ama kusalia katika KANU. Alisema jamii hiyo ilijipata katika baridi 2002 baada kukosa kujipanga vyema.

Towett alishauri jamii ya Kipsigis kutopuuza ushauri wa Moi kwao kuwa wawe waaminifu kwa KANU. Wakati huo, chama cha ODM cha Raila Odinga kilikuwa kimejiuza vyema, japo Moi na chama chake cha KANU waliunga Rais wa wakati huo Mwai Kibaki mkono, kupitia chama chake cha PNU.

Towett alifahamika kwa mazoea yake ya kuvaa miwani kichwani, alikuwa mtu asiyetabirika na ambaye nyakati fulani alifanya mambo ya kimaajabu.

Aidha, alikuwa mtu mcheshi ambaye kila mtu alipozungumza naye, alikuwa wa kuchekesha na kuchangamsha.

Mnamo 1961, alishangaza kwa kutangaza kuwa alikuwa mkabila, akiirai jamii yake ya Kalenjin kujipenda, japo miaka kumi baadaye aliwataja watu wanaopenda jamii zao pekee kama wasioona mbali.

Wakati fulani alipuuzilia shule za bweni kama ambazo zililetwa na wakoloni. Aidha, wakati mfumo wa elimu ya shule za msingi bila malipo ulianzishwa mnamo 2003, aliupuuzilia na kuutaka uondolewe, akisema pesa za kuufadhili zilikuwa nyingi.

Aidha, alikuwa mtu wa kuzungumza mawazo yake, kwani wakati fulani enzi za Uhuru alisema kuwa wezi wanafaa kukamatwa na kupigwa risasi mbele ya umma.

Wakati alipokuwa waziri wa elimu kati ya 1969 na 1979, kulikuwa na hali ya wanafunzi wengi kufeli mitihani ya kitaifa. Kama suluhisho, aliweka tangazo katika vyombo vya habari, akiwataka wanafunzi kutokata tamaa, ila watafute msaada wake.

“Siamini kuwa maisha ya mtu yanafaa kuamuliwa na matokeo ya mtihani. Kila mtu anafaa kupewa fursa kupita mitihani ili awe na maisha mazuri,” akasema katika tangazo hilo.

Ndani ya kipindi cha wiki moja, alikuwa amepokea zaidi ya barua 1,000 kutoka kwa wanafunzi, japo haifahamiki ikiwa aliwahi kuzijibu.

Alikuwa akimiliki magari ya kimaajabu, ambayo ikiwa viti vya wateja havikuwa vimeng’olewa, vilikuwa vimewekwa vikiangalia nyuma, ili gari linapoenda wasafiri badala ya kuangalia mbele wawe wakiangalia nyuma.

Kulingana naye, sababu ya kufanya hivyo ilikuwa kuwa mawazo ya watu wengi huwa kwa namna fulani na hivyo haina haja kuwaangalia usoni, na kuwa dereva hasumbuliwi anapokuwa katika usukani.

Wakati mmoja, alinunua gari jipya aina ya Isuzu Trooper kisha akang’oa viti vya nyuma, badala yake akiweka gunia lililojaa simiti. Dereva wake Mathew Thuita alisema alisisitiza kuwa sharti kiti hicho king’olewe ama kiangalie nyuma.

Miaka michache kabla ya kufa kwake, aliambia wanahabari katika mkahawa mjini Nakuru kuwa alipenda kula chajio usiku wa manane.

Akiwa katika baa, alipenda kujifungulia pombe kwa kutumia kifaa chake, huku akijiwekea vifuniko katika mfuko.

Akieleza sababu ya kufanya hivyo, alisema kuwa hiyo ilimsaidia kuhakikisha kuwa wahudumu wa baa hawangemhadaa baada ya kulewa.

Kila alipohitajika kulipa pombe, angetoa vifuniko hivyo na kuvihesabu ili kujua kiwango cha pombe ambacho alikuwa amekunywa, kabla ya kulipa.

Historia

Alikuwa mwandishi wa filosofia, ambaye aliandika vitabu kuhusu jamii ya Kipsigis, lugha hiyo na maisha ya jamii pana ya Kalenjin, pamoja na historia ya Kipsigis.

Mnamo 1981, alishangaza watu wakati aliposema kuwa alikuwa ameandika wosia kutaka atakapokufa maiti yake itumiwe katika utafiti na Chuo Kikuu cha Nairobi, idara ya masomo ya Udaktari.

Nyumbani kwake, alikuwa amejenga nyumba chini ya ardhi badala ya juu yake. Kulikuwa kukiitwa Mashimoni kwa sababu hiyo.

Alioa mara tano na kutalikiana mara mbili, wawili waliotalikiana ikiwa kwa kukosa kuelewana kuhusu hali yake ya maisha, na ni nani aliyefaa kuishi na wana wao.

Hii ni kwa kuwa aliwahitaji wake na wanawe kutuma maombi kabla ya kutembelea nyumba yake.

Alifariki mnamo Oktoba 8, 2007, wakati ajali ilitokea mtaa wa Free Area, Nakuru.

Alifariki baadaye alipokuwa akitibiwa katika hospitali ya Pine Breeze Nakuru baada ya ajali hiyo.

You can share this post!

Matiang’i akaribishwa Migori kishujaa

DINI: Badala ya kulalamika, utumie muda huo kuyashughulikia...

adminleo