JAMVI: ‘Punguza Mizigo’ kugonganisha madiwani na vigogo wa vyama
Na PETER MBURU
NAIBU Rais William Ruto ameonyesha ishara za wazi kuwa ndiye atakuwa mpinzani mkuu wa wito wowote wa kuandaliwa kwa kura ya maamuzi nchini, baada ya kusema kuwa haoni haja yoyote ya kura hiyo kuandaliwa.
Dkt Ruto alisema kuwa kulingana naye hakuna mabadiliko yoyote ya katiba kwa njia ya refarenda ambayo yataibadilisha Kenya ilivyo sasa, na kusema kuwa ikiwa kuna mabadiliko yoyote yanayohitajika kisheria yanaweza kufanyiwa bungeni.
Akizungumza Jumapili wiki iliyopita, Naibu Rais vilevile alisema haungi mkono pendekezo lolote ambalo litataka kubuniwa kwa serikali ya mseto.
“Sidhani kutakuwa na utunzi wowote wa sheria ama ubadilishaji wa katiba ambao utaibadilisha Kenya kutokuwa nchi ya vyama vingi ilivyo sasa. Baadhi ya mapendekezo ninayosikia watu wakitoa kama wanaoshinda na wanaoshindwa uchaguzini kuingizwa serikalini baada ya uchaguzi nayapinga kwa kuwa huko ni kupendekeza tuishie kuwa na nchi ya chama kimoja.
“Ikiwa hakutakuwa na mshindi katika uchaguzi, tunavyosema ni kuwa tunajaribu kuunda nchi ya chama kimoja. Tunajipeleka moja kwa moja kwa Udikteta,” Dkt Ruto akasema.
Lakini alisema kuwa kulingana naye badiliko linalohitajika ni kuundwa kwa afisi rasmi ya kiongozi wa upinzani ili kustawisha upinzani wa nchi ambao alisema umefifia, badiliko ambalo alisema halihitaji kuandaliwa kwa referenda.
“Changamoto ambayo tuko nayo na ambayo imefifisha upinzani nchini ni kuwa mshindani wa Rais katika uchaguzi hana afisi mahususi. Kwa maoni yangu hilo linahitaji kuweka kipengee kinachowapa viongozi wa upinzani rasilimali za kuendesha majukumu yao, na halihitaji kuandaliwa kwa refarenda. Katiba inaweza kurekebishiwa bungeni kuweka mapendekezo hayo,” akasema Dkt Ruto.
Kiongozi huyo hakupinga mswada wa ‘Punguza Mizigo’ pekee ulioundwa na chama cha Third Way Alliance, ila wowote ambao utapendekeza kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.
Akizungumza kuhusu jopo lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kukusanya maoni ya Wakenya, Building Bridges Initiative (BBI), Ruto alisema lengo la kuundwa kwake halikuwa ili ibadilishe sheria.
“Lengo la kuunda BBI lilikuwa kuunganisha taifa na kuondoa tofauti na chuki dhidi ya makabila na ni hivyo tunavyotarajia ifanye. Haifai kuchukua nafasi ya katiba ama muundo wa kisheria uliopo,” Dkt Ruto akasema.
Alipinga hata pendekezo ambalo Rais Kenyatta alitoa mwaka jana kuwa hakuna haja ya kuwa na chaguzi ambazo watu wanapigania kiwango cha kutenganisha wananchi, ila kinachohitajika ni kujumuisha jamii tofauti uongozini.
“Sharti tubaini njia ya kuwafanya wanaoshiriki chaguzi kuelewa kuwa kutakuwa na mshindi na mshindwa. Tunataka kuwa na hali ambapo watu wanakubali matokeo na uamuzi wa Wakenya.
Msimamo wa kiongozi huyo, hata hivyo, umeonekana kukinzana na ile ya baadhi ya wafuasi wake, ambao aidha wanaunga mswada wa Punguza Mizigo kikamilifu, ama vipengee fulani.
Kiongozi wa wengi Seneti Kipchumba Murkomen ni mmoja wa viongozi ambao wamekuwa wakipigia mswada huo debe, na kuwataka maMCA kuupitisha.
“Madiwani wana fursa ya kipekee kuonyesha mamlaka yao kwa kuunga mswada wa Dkt Ekuru Aukot wa Punguza Mizigo. Kwa muda mrefu wamekuwa wakidharauliwa. Sasa wakumbushe watu kuwa asasi za ugatuzi zina usemi,” Bw Murkomen akasema Julai 21, wakati mswada huo ulipitishwa na Tume ya Uchaguzi IEBC.
Kulingana na baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa, kuna uwezekano Naibu Rais akawa kipau mbele kupinga mwito wowote wa refarenda, sababu kuu ikiwa hadi sasa ndiye mwaniaji mkuu wa Urais katika uchaguzi ujao, na hivyo badiliko lolote linaweza kuathiri uwezekano wake kuingia Ikulu.
Bw Nderitu Wa Ihura anahoji kuwa umaarufu wa Dkt Ruto bado uko juu kwa sasa, lakini katiba ikibadilishwa ili viti kama vya Waziri Mkuu viingizwe, huenda kukaundwa muungano ambao utakuwa maarufu kumshinda Naibu Rais.
“Hivyo kulingana naye, afadhali hali iendelee kuwa kama ilivyo sasa kwani ikienda hivi hadi 2022 uwezekano wake kuwa Rais utakuwa juu. Lakini anafahamu kuwa badiliko la kikatiba kwa njia ya refarenda huenda likayeyusha umaarufu ambao amekuwa akijenga na watu wengine wakaibuka kumpiku,” anasema Bw Ihura.
Wachanganuzi wengine, hata hivyo, wanaona kuwa huenda Naibu Rais akawa na kibarua kigumu mswada wowote kati ya Punguza Mizigo ama BBI ukipenya kufikia hatua ya kura ya maamuzi, kwani huenda akatengwa na wafuasi wake wakiwepo madiwani, wakikimbilia maslahi yao ya kibinafsi.
Tayari ilivyo sasa, kando na seneta Murkomen, seneta wa Nakuru Susan Kihika pia ameeleza kufurahishwa kwake na mswada wa Punguza Mizigo, japo akikosoa vipengee fulani.
“Kuna uwezekano kuwa refarenda ikiandaliwa, wabunge na maseneta watapiga kura na kupigia debe misimamo ambayo wanadhani itawanufaisha wao binafsi. Haitakuwa kwa ajili ya vigogo wao,” anasema Bw Ndegwa Njiru, mdadisi mwingine.