Viongozi wa Magharibi wamlilia Rais awape waziri serikalini
NA SHABAN MAKOKHA
VIONGOZI kutoka Kaunti ya Kakamega wameanzisha juhudi za kumshawishi Rais Uhuru Kenyatta kumteua Waziri kutoka eneo hilo, huku tetesi zikishika kasi kwamba huenda Baraza la Mawaziri likafanyiwa mabadiliko hivi karibuni.
Wanasiasa hao wanadai kwamba eneo hilo halina uwakilishi kwenye baraza hilo, hasa baada ya aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa, kutimuliwa na nafasi yake kutojazwa na mwanasiasa kutoka eneo Magharibi.
Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala, Kiranja wa wengi kwenye Bunge la Kitaifa Benjamin Washiali(Mumias Mashariki), Emmanuel Wangwe(Navakholo) na Bernard Shinali(Ikolomani), ni baadhi ya viongozi wanaoendeleza juhudi hizo, wakisema Rais Kenyatta ameitelekeza jamii ya Waluhya licha ya kupata uungawaji mkono kutoka kwao kwenye uchaguzi wa mwaka 2017.
Kulingana na Bw Wangwe, kuhamishwa kwa aliyekuwa Katibu katika idara ya uhamiaji Gordon Kihalanga hadi Wizara ya Ulinzi hakutoshi kudhihirisha kwamba Rais anawajali watu wa kaunti hiyo na eneo la Magharibi kwa jumla.
“Tumekuwa tukiwaona mawaziri wakiandaa vikao kwenye hoteli kujadili masuala yanayoathiri maeneo yao. Kaunti ya Kakamega inafaa kupokezwa wadhifa wa uwaziri ili kuwezesha masuala yetu kujadiliwa katika mikutano ya baraza la mawaziri,” akasema Bw Wangwe.
Bw Washiali naye alidai kwamba teuzi ambazo zimekuwa zikitangazwa zinawafaidi tu watu wanaounga mkono ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Kinara wa ODM maarufu kama ‘Handisheki’.
Kulingana naye teuzi hizo zinaonyesha wazi kwamba Rais hawajali tena watu kutoka uliokuwa mkoa wa Magharibi ambao wamekuwa wakiunga mkono upinzani lakini walikuwa wameanza kuikumbatia serikali.
“Nataka Rais aelewe kwamba anawadhalilisha wakazi wa Magharibi na hasa kaunti ya Kakamega ambao watu wake walimpigia kura na kumpa viti vinne vya ubunge licha ya mawimbi makali kutoka kwa upinzani. Hii ni dalili tosha kuwa sisi ni sehemu ya serikali ya Jubilee na tuna kila sababu kupata manufaa ya serikali,” akasema Bw Washiali kwenye mkutano mjini Butere.
Hata hivyo, Bw Malala alitofautiana na wabunge hao akisema wao ni wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye anaweza kumfikia Rais kwa urahisi na kumshawishi kuteua waziri kutoka jamii ya Waluhya.
“Wabunge hawa wanaolalamika kwamba waziri anafaa kuteuliwa kutoka jamii yetu wanatoka chama cha Jubilee na ni wandani wa Naibu Rais. Huwa mnajadili nini mkiwa naye? Huwa mnazungumzia tu masuala yenu ya kibinafsi?” akauliza Bw Malala.