BURIANI LABOSO: Saratani sasa janga la kitaifa
VALENTINE OBARA na GEORGE MUNENE
WAKENYA elfu 33 wanafariki kila mwaka kutokana na kansa, ugonjwa ambao Jumatatu ulimuua Gavana Joyce Laboso wa Bomet, siku tatu baada ya kumwangamiza Mbunge wa Kibra, Ken Okoth.
Kulingana na Waziri wa Afya, Bi Cecily Kariuki, kila mwaka kuna maambukizi mapya elfu 48 ya saratani aina mbalimbali yanayogunduliwa nchini.
Kando na maelfu ya raia wa kawaida wanaofariki katika kila pembe ya nchi kutokana na ugonjwa huo ulio vigumu kutibiwa, orodha ya viongozi na watu mashuhuri waliokufa kwa kansa inaendelea kuwa ndefu.
Mijadala imekuwepo bungeni, Serikali Kuu na miongoni mwa magavana kuhusu mikakati inayofaa kuwekwa ili kuzuia maangamizi haya ya saratani yanayoshuhudiwa kila mara.
Lakini hakuna hatua kubwa ambazo zimepigwa kufikia sasa, na raia wengi wa kawaida wanaendelea kufariki baada ya kutumia mamilioni wakitafuta matibabu nje ya nchi hasa India.
Bi Kariuki alisema hali imekuwa mbaya sana na akaagiza vituo vyote vinane vya kutibu kansa nchini vianzishe mara moja uchunguzi wa kimatibabu na matibabu ya kina kwa ugonjwa huo.
“Tunataka wale wanaougua ugonjwa huu waanze kutibiwa mapema ili kupunguza idadi ya wanaofariki. Kansa ni janga ulimwenguni kote na husababishwa na jinsi watu wanavyoishi maisha yao ya kila siku,” akasema Bi Kariuki.
Waziri huyo alikuwa akizungumza katika kijiji cha Mutuavare, Kaunti ya Embu ambako alisambaza chakula cha msaada kwa wakazi.
“Wakenya wanafaa wawe waangalifu kwa kile wanachokula ili wajiepushe na maradhi ya kansa na waishi maisha marefu,” akaongeza.
Mbali na kukosa kufanya mazoezi, inahofiwa vyakula hatari vilivyojaa sumu ambavyo vimekuwa vikigunduliwa nchini vimechangia pakubwa katika ongezeko la watu wanaofariki kwa maradhi hayo.
Kumekuwa na ripoti za nyama iliyowekwa dawa zenye sumu, mchele na sukari ulio na madini hatari ya mercury, pombe zenye sumu na matumizi ya kemikali hatari kwenye kilimo, huku Serikali ikishindwa kuhakikishia Wakenya ubora wa vyakula kutokana na ufisadi na mifumo duni ya udhibiti.
Dkt Laboso amekuwa gavana wa tatu kufariki akiwa mamlakani, baada ya Gavana wa Nyeri Wahome Gakuru ambaye alikufa kwa ajali barabarani mnamo 2017, na mtangulizi wake Nderitu Gachagua aliyeugua kwa muda mrefu.
Kulingana na Katiba, Naibu Gavana wa Bomet, Bw Hillary Barchok atachukua mamlaka hadi uchaguzi mkuu ujao utakapofanywa.
Mapema mwezi huu, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Bw Bob Collymore naye pia alifariki kwa saratani. Mnamo Mei, aliyekuwa Karani wa Bunge la Taifa, Bw Justin Bundi alifariki baada ya kuugua ugonjwa huo.
Alipoenda kufariji familia ya Dkt Laboso katika hifadhi ya maiti ya Lee, Kaunti ya Nairobi, Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga alisema kunahitajika mikakati kama vile ujenzi wa vituo zaidi vya matibabu ya saratani katika kila kaunti.
“Ulimwenguni kote, imebainika kansa ikigunduliwa mapema kabla isambae zaidi mwilini inaweza kutibiwa. Wananchi wanafaa kwenda kupimwa lakini kwa bahati mbaya hatujaweza kupata vituo vya kutosha vya kutibu saratani,” akasema.
Mswada wa kuhakikisha kila kaunti itajenga kituo cha matibabu ya saratani ungali bungeni.
Baraza la Magavana hushinikiza serikali kuu kutoa rasilimali zaidi kwa serikali za kaunti kuboresha huduma za matibabu ya kansa kwa kila kaunti ili wananchi wasilazimike kusafiri hadi Nairobi kutafuta huduma hizo.
Mijadala kuhusu yanayopasa kufanywa kukabiliana na janga la saratani hupamba moto kila mara mtu maarufu anapoaga dunia kutokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo bado hakujakuwa na hatua madhubuti za kupiga breki maangamizi ya ugonjwa huo ambao athari zake zimesambaa katika familia nyingi, uchumi na jamii kwa jumla.