• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Rotich na wenzake wabebe misalaba yao – Viongozi Kimwarer

Rotich na wenzake wabebe misalaba yao – Viongozi Kimwarer

Na BARNABAS BII

VIONGOZI kutoka eneo la Kerio Valley ambapo mabwawa ya Arror na Kimwarer yalifaa kujengwa wanataka watu walioshtakiwa kuhusiana na sakata ya wizi wa fedha zilizotengewa miradi hiyo kubeba misalaba yao.

Viongozi hao wakiongozwa na Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos waliitaka serikali kuhakikisha kwamba fedha hizo zinarejeshwa ili shughuli ya ujenzi wa miradi hiyo ya thamani ya Sh63 bilioni ianze.

“Wengi walitarajia kufanyika kwa maandamano baada ya washukiwa wakuu katika sakata hiyo kukamatwa lakini hilo halikufanyika. Tunachotaka ni kurejeshwa kwa fedha hizo ili mradi huo uwanufaishe wakazi,” akasema Tolgos alipokuwa akizungumza katika eneo la Chesongoch, Marakwet Mashariki.

Alisema washukiwa wakuu wa sakata ya mabwawa wachukuliwe hatua kali bila kujali nyadhifa zao serikalini.

“Kuna uwezekano kwamba kuna wakuu serikalini walionufaika na sakata hiyo na pia kuna baadhi ya washukiwa ambao hawajui lolote kuhusiana na wizi huo. Sheria iadhibu waliohusika na wasio na hatia waachiliwe huru,” akasema Bw Tolgos.

Alieleza kwamba mradi huo wa mabwawa ungeinua hali ya uchumi ya wakazi wa eneo la Kerio.

Miongoni mwa wakazi wa eneo hilo ambao wameshtakiwa kuhusiana na sakata hiyo ni waziri wa Fedha Henry Rotich ambaye tayari amesimamishwa kazi, David Kimosop ambaye ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawi wa eneo la Kerio (KVDA), na Mkurugenzi Mtendaji wa KVDA Francis Kipkech.

Wengine walionaswa kuhusiana na sakata hiyo ni Katibu wa Wizara ya Afrika Mashariki Susan Jemtai Koech na Katibu wa Wizara ya Fedha Kamau Thugge kati ya wengine.

Bwawa la Arror lililofaa kugharimu Sh35 bilioni liko katika eneo la Marakwet Magharibi na lile la Kimwarer lenye thamani ya Sh28 bilioni liko Keiyo Kusini.

Kampuni ya CMC di Ravena ya nchini Italia ndiyo ilipewa kandarasi ya kujenga mabwawa hayo mawili makubwa eneo la Bonde la Ufa.

You can share this post!

Wazee waficha mvi wasiuawe

Wagiriama warejeshewa sanamu zilizokuwa zimefichwa Uingereza

adminleo