• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
GWIJI WA WIKI: Jackline Mshingo

GWIJI WA WIKI: Jackline Mshingo

Na CHRIS ADUNGO

HAKUNA yeyote aliye na nguvu za kuizima ndoto yako isipokuwa wewe mwenyewe! Usikubali kukatishwa tamaa na wabinafsi wachache utakaokutana nao maishani.

Huwezi kujenga chochote bila ramani. Tambua kipaji chako na upange vyema jinsi unavyotumia muda wako. Unapoanza kujilinganisha au kuilinganisha kazi yako na za watu wengine; matokeo yake ni kwamba utaanza kujidharau, kujihukumu, kujiona asiyefaa au asiyeweza kufanya jambo lolote la maana.

Kila mtu aliumbwa afanye kitu kilicho tofauti na mwingine na kwa njia zisizofanana. Sote tuna mitindo tofauti inayotutambulisha katika fani mbalimbali. Kumbuka mafanikio ni zao la imani, jitihada na nidhamu. Thamini kile unachokifanya huku ukijitahidi kwa jino na ukucha kuwa bora.

Huu ndio ushauri wa Bi Jackline Mshingo ambaye kwa sasa ni Mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Good Testimony, Nairobi.

Maisha ya awali

Jackline alizaliwa mtaani Tudor, Mombasa katika familia ya mwalimu mstaafu Bi Elizabeth Wachia na marehemu Bw William Kongoda ambaye hadi kufariki kwake alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli la Kenya. Baada ya kupata elimu ya chekechea shuleni Railways, Tudor, Jackline alijiunga na Shule ya Msingi ya Marycliff, Tudor alikosomea hadi darasa la sita.

Mnamo 1978, Bi Wachia alipata uhamisho mpaka St Joseph’s Ngerenyi katika eneo la Wundanyi, Kaunti ya Taita-Taveta. Hivyo, ilimjuzu Jackline kujiunga na Shule ya Msingi ya Ngerenyi alikofanyia mtihani wa kitaifa wa CPE mwishoni mwa 1979.

Alama nzuri alizozipata zilimpa fursa ya kujiunga na Shule ya Upili ya Coast Girls, Mombasa mnamo 1980 na akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari mwishoni mwa 1983.

Jackline anakiri kwamba kifo cha baba yake mzazi kilichotokea mnamo 1984 kiliyumbisha pakubwa ulimwengu wake, kubadili sana maisha yake na kutikisa mno nyingi za ndoto zake kwa kuwa ni jambo lililotishia kuzima kabisa mshumaa wake wa elimu.

Mtihani mgumu ambao alikabiliana nao baada ya sekondari ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwanahabari maarufu au mwalimu mashuhuri wa Kiswahili.

Hizi ni taaluma ambazo alivutiwa nazo tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Ualimu

Kwa imani kwamba penye mawimbi na milango i papo hapo, Jackline alianza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Kirindinyi, eneo la Mbololo, Taita mnamo 1985. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Mnamo 1988, mkoko ulianza kualika maua maishani mwake pindi alipojiunga na Chuo cha Walimu cha Asumbi, eneo la Suneka, Kaunti ya Homa Bay. Alifuzu mwishoni mwa Julai 1990 na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ikamtuma kufundisha katika Shule ya Msingi ya Mkwachunyi, Mbololo.

Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Miasenyi, eneo la Maungu, Taita. Mnamo 1991, alifunga pingu za maisha na Bw Hautom Mshingo (kwa sasa marehemu) na kupata uhamisho hadi Shule ya Msingi ya Makupa, Mombasa. Alihudumu huko kwa miaka mitatu kabla ya kuelekea jijini Nairobi kufundisha Shule ya Msingi ya Lang’ata Road kati ya 1994 na 2002.

Mnamo 2003, alijiunga na Shule ya Msingi ya Lang’ata Barracks, Nairobi na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Pia alichaguliwa kuwa msimamizi wa Kiswahili, Katibu wa michezo katika gatuzi dogo la Lang’ata na mwanajopo wa kutunga mitihani katika Kaunti ya Nairobi.

Jackline aliwahi pia kuwa mshauri wa Taasisi ya Uratibu wa Mitaala na Masomo (KICD) kuhusu masuala ya Kiswahili kati ya 2008 na 2011.

Katika kipindi cha miaka tisa ya kuhudumu kwake shuleni Langata Barracks, Jackline alivumisha zaidi matokeo ya somo la Kiswahili na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa lugha hiyo miongoni mwa wanafunzi.

Akiwa huko, pia alifundisha shule nyingi za kibinafsi jijini Nairobi na kutangamana na waandishi, wanahabari na walimu mbalimbali waliowasha moto wa azma ya wanafunzi wake kukichapukia Kiswahili.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ni kiini cha Jackline kujiunga na Kampala International University (KIU) kusomea ualimu (Kiswahili na Historia) kati ya 2007 na 2010.

Ilikuwa hadi 2013 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), Nairobi kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa elimu.

Kujiuzulu

Mnamo Januari 2011, Jackline alikatiza uhusiano na TSC na kujiunga na Shule ya Msingi ya Anthena, eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos. Akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na pia Mwalimu Mkuu, Anthena School ambayo kwa sasa ipo chini ya ukurugenzi wa Bw Otuche Adidi na Bi Josephine Adidi, ilisajili alama wastani ya 379.83 katika mtihani KCPE 2016 baada ya wanafunzi kujizolea alama wastani ya 81.73 katika Kiswahili.

Mnamo 2017, alama wastani ya 75.05 iliyovunwa na watahiniwa wa Anthena katika somo la Kiswahili ilichangia pakubwa alama wastani ya 354.54 iliyosajiliwa na shule hiyo katika mtihani wa KCPE.

Jackline anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote katika somo lolote kunategemea mtazamo wake kuhusu somo husika na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa yenyewe darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Good Testimony kwa sasa ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaotazamia kuvuna matokeo ya KCPE 2019 yatakapotolewa.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuimarisha zaidi viwango vya usomaji na ufundishaji wa Kiswahili nchini, Jackline anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Amechangia pakubwa kuinua sekta ya elimu katika Kaunti ya Taita-Taveta kwa kushirikiana vilivyo na aliyekuwa Waziri wa Elimu katika gatuzi hilo, Bi Jemimah Tuja mnamo 2013. Jackline pia ameandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujizatiti kwa mitihani ya KCPE.

Amejaliwa binti, Cecilia Sanguli ambaye kwa sasa ni mfanyakazi wa Halmashauri ya Ushuru ya Kenya (KRA) na mkewe mwigizaji Bw Blessing Lung’aho wa kipindi Mother-In-Law katika runinga ya Citizen.

You can share this post!

Kipusa awaka kupata sketi kitandani

WASIA: Namna ya kukabili kiherehere cha mtihani ili kuvuna...

adminleo