Mastaa 9 wajumuishwa katika kikosi cha Harambee Stars
Na GEOFFREY ANENE
WACHEZAJI wote tisa wanaopiga soka nchini walioitwa na kocha Stanley Okumbi wamefanikiwa kuunda timu ya taifa ya Harambee Stars itakayomenyana na Comoros na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) hapo Machi 24 na Machi 27, mtawalia.
Walielekea nchini Morocco mnamo Machi 19 kuungana na wachezaji wa kimataifa kwa mechi hizo mbili za kirafiki.
Kipa bora wa mwaka 2017 Patrick Matasi (Posta Rangers) atasaidiana michumani na John Oyemba (Kariobangi Sharks) na Faruk Shikalo (Bandari).
Nahodha wa Gor Mahia, Harun Shakava ndiye beki wa pekee anayetandaza soka nchini amepata namba katika kikosi cha Okumbi.
Viungo wanaopiga soka humu nchini waliojumuishwa kikosini ni Patilah Omoto kutoka Kariobangi Sharks, Francis Kahata (Gor Mahia), Duncan Otieno (AFC Leopards) na Samuel Onyango.
Mshambuliaji Erick Kapaito yumo mbioni kuchezea Kenya kwa mara ya kwanza kabisa. Amekuwa katika hali nzuri kwenye Ligi Kuu akifungia Sharks mabao matano katika mechi saba.
Okumbi hajatema mchezaji yeyote katika kikosi cha wachezaji 24 alichoita Machi 9 kwa mechi hizo zitakazopigiwa mjini Marrakech.
Orodha ya wachezaji wanaosakata soka ya malipo nje ya Kenya inajumuisha mabeki Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), David Ochieng, (IF Brommapojkarna, Uswidi), David Owino (Zesco, Zambia) na Abud Omar (Slava Sofia, Bulgaria).
Victor Wanyama kutoka Tottenham Hotspur nchini Uingereza anaongoza orodha ya viungo, ambayo pia iko na Athuman Ismael Gonzales (CF Fuenlabrada) na McDonald Mariga (Real Oviedo) wote kutoka Uhispania, Anthony Akumu (Zesco, Zambia), Johanna Omollo (Cercle Brugge KSV, Ubelgiji), Paul Were (FC Kaisar, Kazakhstan), Eric Johana Omondi (IF Brommapojkarna, Uswidi). Mariga, ambaye ni kakake Wanyama, hajachezea Stars kwa karibu miaka mitano.
Washambuliaji wa kimataifa ni Ayub Timbe (Heilongjiang FC, Uchina), Cliffton Miheso (Buildcon FC, Zambia), Jesse Were (Zesco FC, Zambia) na Michael Olunga (Girona FC, Uhispania).
Shirikisho la Soka duniani (FIFA) huruhusu wachezaji wa kimataifa kujiunga na timu zao za taifa siku tano kabla ya mechi kwa hivyo Wanyama na wenzake wanatarajiwa nchini Morocco wakati wowote.
Kenya inashikilia nafasi ya 105 katika viwango bora vya FIFA vilivyotangazwa Machi 15. Jamhuri ya Afrika ya Kati na Comoros ziko katika nafasi za 121 na 132, mtawalia.