• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
SEKTA YA ELIMU: Likizo ni awamu muhimu mno katika elimu ya mwanafunzi

SEKTA YA ELIMU: Likizo ni awamu muhimu mno katika elimu ya mwanafunzi

Na CHARLES WASONGA

SHULE zinafungwa wiki hii baada ya kukamilika kwa muhula wa pili.

Wanafunzi wanatarajiwa kusalia nyumbani kwa kipindi cha majuma manne.

Kulingana na kalenda ya masomo ya mwaka huu, wanafunzi watarejelea masomo mnamo Septemba 3, 2019, kuanza muhula wa tatu ambao ni wenye umuhimu, hasa kwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) na ule wa darasa la nane (KCPE).

Kwa mujibu wa ratiba ya mitihani hiyo ya kitaifa iliyotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) mwezi Juni, mtihani wa KCPE utaanza mnamo Oktoba 28 kwa karatasi ya Hisabati na kutamatishwa Oktoba 31 kwa karatasi ya Elimu ya Jamii na Dini.

Watahiniwa wa KCSE wataanza mtihani huo mnamo Novemba 4 na kuukamilisha mnamo Novemba 27.

Kwa hivyo, inatarajiwa kuwa watahiniwa watatumia muda mwingi wakati wa likizo kudurusu kama sehemu ya kujitia makali kwa mitihani hiyo ambayo itatumiwa kuamua mustakabali wao kimasomo.

Hata hivyo, wazazi na walimu wanapaswa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawa pamoja na wenzao wa madarasa ya nyuma wanapumzika wakati huu wa likizo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Msingi ya 2013, likizo ni wakati ambapo wanafunzi hupata fursa ya kupumzika huku wakitangamana na familia, jamaa na marafiki zao nje ya mazingira ya shule.

Huu ni wakati ambapo wazazi nao hupata fursa ya kuchambua rekodi za masomo za watoto wao kubaini changamoto zinazowakumba na kuratibu mbinu za kuzishughulikia shule zinapofunguliwa.

Muhimu zaidi ni kwamba likizo huwa ni wakati mwafaka kwa wazazi na wanajamii kuwafundisha, kuwashauri na kuwaelekeza watoto wao kuhusu maadili.

Kulingana na watalaamu wa elimu, masomo ya darasani yanafaa kuoanishwa na mafunzo ya nyumbani ili baada ya wanafunzi kukamilisha masomo hayo watakuwa watu ambao wanaweza kutumia elimu waliyopata shuleni kuboresha maisha yao na jamii kwa jumla.

Kuwasaidia wanafunzi wenye udhaifu

Hii ndiyo maana serikali ilipiga marufuku masomo ya ziada mwaka wa 2012 baada ya kubainika kuwa walimu waligeuza shughuli hiyo kuwa njia ya kujipatia pesa zaidi wala si kuwasaidia wanafunzi dhaifu kimasomo au kukamilisha silabasi.

Baadhi ya wazazi nao walitumia masomo ya ziada kama kisingizio cha kukwepa wajibu wao kuwa walezi, washauri na waelekezi wa watoto wao hali ambayo imechangia baadhi ya wanafunzi kuwa watundu.

Matokeo yake ni visa vya utovu wa nidhamu ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika shule za upili, haswa muhula wa pili.

Katika uchunguzi ulioendeshwa na lililokuwa jopokazi lililoongozwa na mkuu wa mkoa wa kati Bi Claire Omollo mnamo 2016, ukosefu wa malezi na ushauri wa wazazi ni mojawapo ya sababu kuu zilizochangia visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili mwaka huo. Jumla ya shule 110 za upili ziliteketezwa mwaka huo, wahusika wakuu wakiwa wanafunzi.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Ex wake anamtia presha warudiane,...

MAPITIO YA TUNGO: ‘Usiku wa Mashaka’ ni riwaya...

adminleo