KAULI YA MATUNDURA: Tathmini ya ufaafu wa ‘mzungumzishi’ kwa vigezo vya kinadharia ya Kiisimu
Na BITUGI MATUNDURA
KATIKA makala yangu juma lililopita nilidai kwamba pendekezo la istilahi ‘mzungumzishi’ iliyoubuniwa na seneta maalum – Dkt Agnes Zani haikufaa kwa maana ya ‘spika’.
Hata hivyo, nilimpa kongole Dkt Zani kwa kuthubutu kuisukuma mbele nadharia ya upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ya kuikuza lugha hii ‘mumo kwa mumo’.
Katika makala ya leo, ninajadili ni kwa nini istilahi ‘mzungumzishi’ haifai kwa tathmini ya kinadharia. Nadharia ya kupanua msamiati wa Kiswahili ‘mumo kwa mumo’ ilipigiwa upatu sana na hayati Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa.
Alidai kwamba kabla ya kukimbilia kutohoa au kukopa maneno kutoka kwenye lugha za kigeni, ni muhimu tuchakurechakure kanzi ya maneno katika lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu. Ikiwa tutakosa kabisa neno linaloweza kutumiwa kurejelea dhana ngeni, basi neno libuniwe kwa kuchunguza sifa za dhana ile mpya.
Mimi ninafikiri kwamba mawazo ya kiutendaji ya Dkt Zani yalikuwa yameulenga mkondo huu – ingawa hayakuwa na msingi wa kujikita na ushawishi wa kutosha.
Hatua ya kwanza katika kubuni msamiati au istilahi ni kuwepo haja ya msamiati au istilahi hiyo.
Hapakuwa na haja ya istilahi ‘mzungumzishi’ kwa sababu tayari tuna neno ‘spika’, hili limezoeleka na wasemaji wa Kiswahili na hata kutomeshwa kwenye kamusi.
Profesa Kibuka Kiingi (Uganda) alibuni nadharia ya PEGITOSCA. Anapendekeza kwamba istilahi inayobuniwa ni sharti itimize vigezo vifuatavyo vya PEGITOSCA: Precision (Udhahiri), Economy (Iktisadi), Generativity (Uzalishi), Internationality (Umataifa), Transparency (uwazi), anti-Obsenity (Isomatusi), Systematicity (Umfumo), Consistency (Uangavu) na Acceptability (ukubalifu).
Kimsingi, kila istilahi inayobuniwa sharti iwe dhahiri, fupi na isiyokanganya, iweze kuzaa istilahi nyingine kwa njia ya kunyambuliwa, ikubalike kimataifa, iwe angavu (bila ugiligili), ikubalike kwa urahisi na isisheheni fahiwa ya matusi.
Katika Kiswahili kwa mfano, tuna maneno ‘runinga’ na televisheni ambayo yanatumiwa kama visawe. Ingawa yote mawili yamekubaliwa, ‘televisheni’ ina umataifa zaidi kuliko ‘runinga’.
Aidha, tuna ‘kompyuta’ na ‘tarakilishi’. Ingawa ‘kompyuta’ ni istilahi yenye umataifa zaidi kuliko ‘tarakilishi’, la pili (tarakilishi) linatimiza kiwango cha uzalishi zaidi hivi kwamba linaweza kunyambuliwa na kuunda istilahi nyingi.
Kwa mfano ‘tarakilishia’ (compute for), ‘tarakilishiana’ (compute for one another), ‘nitarakilishie’ (compute for me), tarakilishatarakilisha (compute repeatedly) na kadhalika.
Umataifa
Je, istilahi ‘mzungumzishi’ inatimiza baadhi ya vigezo hivi? Dhana ‘spika’ ina umataifa zaidi kuliko ‘mzungumzishi’.
Kadhalika ‘mzungumzishi’ inakiuka kigezo cha ‘iktisadi’ kwa misingi kuwa neno lenyewe linahitaji kani au nguvu nyingi mno kulitamka.
Maseneta, wakiongozwa na Bw James Orengo walishindwa kabisa kulitamka neno ‘mzungumzishi’ na hiyo ni ishara ya wazi kwamba limekiuka kigezo cha kinadharia cha ‘ikitisadi’ katika lugha.
Vilevile ‘mzungumzishi’ haina uangavu kwa misingi kuwa inazua fahiwa ya kufanyiza na kulazimisha. Kutokana na kitenzi ‘zungumza’ tunaweza kupata maneno kama ‘mzungumziwa’, ‘mzungumzaji’, ‘mzungumzishi’ na kadhalika – nako kumfanya mtu azungumze – yaani ‘kumzungumzisha’ kunaleta dhana ya kutumia nguvu.