Matumaini kwa Amerika kumaliza ukame wa miaka 32 bila taji Boston Marathon

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Marekani wana matumaini makubwa ya kumaliza ukame wa miaka 32 bila taji la mbio za Boston Marathon watakapowakilishwa na Shalane Flanagan, Molly Huddle, Jordan Hasay na Desiree Linden hapo Aprili 16, 2018.

Tangu mwaka 2000, Kenya imeshinda taji la wanawake la Boston mara 12 ikiwemo mwaka 2017 kupitia Edna Kiplagat, Ethiopia mara nne na Urusi mara moja.

Lakini, baada ya Flanagan kuwa Muamerika wa kwanza kutwaa ubingwa wa mbio za New York City Marathon tangu mwaka 1977 aliposhinda makala ya mwaka 2017, Marekani inamini inaweza kupambana na miamba wa mbio ndefu Kenya na Ethiopia.

“Tunaweza kukimbia na Wakenya. Tunaweza kukimbia na Waethiopia. Nadhani orodha ya wakimbiaji wanawake kutoka Marekani wanaoshiriki Boston Marathon mwaka huu wana moyo,” tovuti ya CBS Boston imenukuu bingwa wa New York City Marathon mwaka 1974, Kathrine Switzer, akisema.

Linden alimaliza Boston Marathon katika nafasi ya pili mwaka 2011.

Flanagan amekamilisha makala matatu yaliyopita ya Boston Marathon katika nafasi 10 za kwanza ikiwa ni pamoja na kutimka kasi ya juu kuwahi kukimbiwa na Muamerika mjini Boston alipomaliza makala ya mwaka 2014 katika nafasi ya sita kwa saa 2:22:02.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 36 alikuwa ametangaza atastaafu asiposhinda New York City Marathon mwaka 2017, lakini baada ya kunyakua taji ana kiu ya kupata ufanisi zaidi. Hasay alimaliza marathon za Boston na Chicago katika nafasi ya tatu mwaka 2017.

Itakuwa mara ya kwanza kabisa Huddle kushiriki mbio za Boston Marathon, ambazo mwaka huu zitaadhimisha miaka 122 tangu zianzishwe.

Kiplagat atatetea taji lake. Bingwa wa Boston Marathon mwaka 2015, Caroline Rotich kutoka Kenya pia yuko katika orodha ya washiriki.

Habari zinazohusiana na hii

Hofu ya ghasia Amerika

Amerika yaamua