• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Gavana alilia bunge liteme mawaziri wake watatu

Gavana alilia bunge liteme mawaziri wake watatu

BARNABAS BII na TOM MATOKE

GAVANA wa Nandi Stephen Sang amewarai madiwani kupiga kura ya kutokuwa na imani na mawaziri wake watatu ambao wamehusishwa na kupotea kwa Sh200 milioni.

Kiongozi huyo jana aliwaomba madiwani hao kuwaondoa afisini Waziri wa Barabara Hillary Rotich, mwenzake wa Ardhi Stanley Baliach na Valentine Chumo wa Elimu.

“Njia ya kuwaondoa mawaziri afisini ni wazi kulingana na katiba. Ni kupitia kura ya kutokuwa na imani nao na Bunge la kaunti linafaa kuharakisha kuondolewa kwa mawaziri hawa watatu,” akasema Bw Sang’.

Watatu hao ni kati ya maafisa 12 wa kaunti aliowasimamisha kazi miezi mitatu iliyopita kufuatia malalamishi ya wabunge, madiwani na wenyeji kuhusu kukithiri kwa ufisadi kwenye kaunti hiyo.

Hata hivyo, afisa mkuu wa barabara na miundombinu Johan Biwott alisema ni shahidi kwenye tukio la kupotea kwa magurudumu na vifaa vya ujenzi wa shule 60 za chekechea.

Bw Sang’ pia aliwalaumu mawaziri hao kwa uongozi mbaya uliochangia kupotea kwa mali ya umma.

“Napendekeza mawaziri hao watatu watimuliwe baada ya kupitia ripoti tatu tofauti za uchunguzi. Nawaomba wawakilishi wadi waongeze kasi ya kuwaondoa afisini,” akaongeza Bw Sang’.

You can share this post!

Kampuni za kamari ziruhusiwe kuendelea kuhudumu –...

Kibaki alivyofichwa ndani ya stoo chafu serikali...

adminleo