AKILIMALI: Mfanyakazi wa kaunti anayepiga jeki pato kupitia ukulima, ufugaji
Na LUDOVICK MBOGHOLI
JOHN Mbai ni miongoni mwa maafisa wachache wa kaunti ya Taita Taveta wanaofanya kazi kwenye kaunti ndogo ya Taveta, ambao wanazingatia shughuli za ukulima na ufugaji.
Afisa huyu sasa anahudumu kwa mwaka wa 20 akiwa mtoza ushuru, hasa akiwatoza wafanyabiashara wenye maduka ya kuuza nyama (bucha) sawa na wanaomiliki vichinjio vya mifugo.
Aidha ni afisa anayechukua jukumu la kuhakikisha wachinjaji sawa na wachunaji wa mifugo waliochinjwa wanalipwa malipo yao.
Kadhalika anashughulikia malipo ya madaktari wanaokagua mifugo wanaoletwa kichinjioni, ili kuhakikisha mifugo hao ni salama na wenye afya njema kabla ya kuchinjwa.
Kwa wakati huu John Mbai anawajibikia pia ufugaji wa kuku licha ya kushughulikia ukulima wa mazao ya nafaka sawa na ndizi.
“Mimi ni mkulima mfugaji mwenye shamba la wastani, ambalo nalima mazao ya nafaka kama mahindi, maharagwe na mboga mbali na matunda. Lakini kwa kuwa ndizi ni zao maalumu la kibiashara hapa Taveta, inabidi nilizingatie kwa kutunza miche ya migomba nikilenga kuipanda,” Mbai aambia Akilimali kwenye mahojiano.
Hata hivyo, shughuli za ukulima wa mazao hazikuvunja azma yake ya ufugaji.
“Hata kama nalima mazao ya vyakula vya nafaka na ndizi shambani kwangu, ukulima huo hauwezi kunizuia kuzingatia ufugaji wa kuku ambao naupenda mno,” aarifu Mbai huku akisema alianza ufugaji wa kuku kwa vifaranga 100 (wa mwezi mmoja).
Tarehe mosi ya mwezi Machi mwaka huu aliwaleta vifaranga hao na kuanza shughuli hii.
“Kuku ninaofuga hapa ni aina ya Rainbow Rooster na wa kienyeji. Baada ya mauzo nimesalia na kuku 93 aina ya Rainbow Rooster na zaidi ya 170 wa kienyeji,” anaelezea zaidi afisa huyu wa serikali ya kaunti.
Hata hivyo, kwenye mahojiano yake na Akilimali, Mbai anasema kuna changamoto tele anazokumbana nazo kila uchao.
“Nataabika kupata chakula chao. Inalazimu niagize chakula aina ya Kienyeji Mash kutoka mjini Mombasa na chakula kingine cha mchanganyiko wa pumba, dagaa na mashudu kutoka huko Holili nchini Tanzania,” anaelezea.
Aidha, afisa huyu anafichua kuwa jinsi ya kuwalisha kuku hao inamtegemea pakubwa kwani ni lazima ahakikishe hakuna hata kuku au kifaranga mmoja anayekosa mahitaji yake.
“Ni lazima mimi mwenyewe niwepo kwenye shughuli ya kuhakikisha lishe yao inakidhi mahitaji. Mimi huwalisha mara tatu kwa kila wiki, lakini nikiachia mtu mwingine anashindwa kufanya hivyo na badala yake walishwe mara mbili au moja kwa wiki,” apasha zaidi mfugaji huyu.
Huagiza kilo 50 za chakula cha kienyeji (mash) kutoka Mombasa kwa Sh1,500 na chakula cha mchanganyiko wa pumba, dagaa na mashudu kutoka Tanzania kwa Sh1,000.
“Nagharamika kila wiki Sh2,500 kwa chakula. Hata hivyo natarajia kuongeza idadi ya kuku hawa, nitaleta wengine 200 wa mayai na 100 wa nyama,” anasema afisa huyu.
Kiwango cha maji
Kadhalika, Mbai anadokeza kuwa kuku wake hunywa lita 20 za maji mara nne kila siku.
Hali inayomlazimu kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa hata ikiwa hayuko nyumbani.
“Mara nyingi mimi hushindia kazini, lakini ni lazima nihakikishe maslahi ya kuku wangu yanatekelezwa. Wanakunywa lita 20 za maji mara nne kila siku, hivyo inabidi hata nikiwa kazini nimuulize mke wangu kama wamepewa maji,” asisitiza.
Na licha ya kunywa maji lita 20 mara nne kwa siku, inabidi kila saa wabadilishiwe maji ili wasipate maradhi ya maambukizi licha ya kukaguliwa na madaktari.
“Wanapewa maji mara nne kwa siku lakini pia yanabadilishwa mara nne,” Mbai alielezea Akilimali.
Alipoulizwa ni vipi anaweza kumudu majukumu ya kiofisi na ya ufugaji mtawalia, afisa huyu alikiri zipo changamoto si haba.
“Inabidi nifanye kazi masaa mengi ya ziada ili niyafidie kwenye mapumziko ya dharura ndani ya wiki au wikendi. Wakati huo ndio napata nafasi ya kuwahudumia,” asadikisha afisa huyu.