Habari

PhD: JKUAT yatoa msimamo wake

August 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology (JKUAT), kimetoa taarifa yake kuhusu msimamo wao kuhusu utata unaoendelea wa kufuzu kwa wasomi 118 waliopata shahada za uzamifu (PhD), mwezi mmoja na nusu uliopita.

Chuo hicho kimesoma ripoti ya Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) ambapo kamati ya seneti inafuatilia ripoti hiyo kwa makini.

Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Victoria Wambui Ngumi, alizidi kufafanua kuwa baada ya kamati hiyo ya Seneti kupitia ripoti hiyo, itawasilisha mawazo hayo kwa Wizara ya Elimu na afisa mkuu mtendaji wa CUE chini ya muda wa miezi mitatu.

Chuo cha JKUAT kimegundua ya kwamba mengi yamesemwa kuhusu shahada hizo za uzamifu ambapo mengi yamejadiliwa na umma huku vyombo vya habari vikiangazia kuhusu swala hilo.

Hata hivyo, alisema hakuna shahada yoyote kati ya hizo 118 imefutiliwa mbali.

Katika hotuba yake kwa waandishi wa habari aliyoisoma mnamo Jumatano katika chuo hicho, Prof Ngumi alitoa hakikisho ya kwamba shahada zote zinazokabidhiwa wanafunzi wote huwa zimefanyiwa kazi kwa kufanya mitihani, kupitia mikutano na utafiti wa kina na huku wakiendesha mitihani ya ndani ya chuo na kufuata mtindo wa maadishi unaostahili.

Aliendelea kukiri ya kwamba masomo yanayofunzwa JKUAT ni ya hali ya juu na angetaka kila Mkenya aelewe ya kwamba kuna wahadhiri waliosoma wenye vyeti vya hadhi ya juu zaidi.

Alitaja utafiti katika masomo tofauti pia ni wa hali ya juu.

Alifafanua kuwa chuo hicho kiko katika ubora wa ISO 9001:2015 kategoria ya Quality Management System na pia ubora wa ISO 14001:2015  kategoria ya Enviromental Management System.

Alieleza ya kwamba utata wote wa maswala hayo ulishuhudiwa mnamo Juni 21, 2019, wakati wa kufuzu kwa wahitimu 3,545 katika hafla ya 33 iliyoshuhudiwa wakati huo.

Mnamo siku hiyo wasomi wapatao 118 walitunukiwa shahada za juu zaidi za uzamifu (PhD), jambo lililozua utata kupitia Wizara ya Elimu.

Baadaye wizara ilitoa amri CUE ifanye uchunguzi zaidi kuthibitisha kama kweli vyeti vilivyotolewa vilikuwa halali au la.

Wakenya wengi ilidaiwa walishangazwa na tukio hilo kwani wengi hawajawahi kusikika idadi kubwa ya wasomi wakifuzu kama ilivyotokea.

Prof Ngumi alisema kwa muda wa wiki chache zijazo ripoti kamili itatolewa na Wakenya watapata ukweli wa mambo.