Habari Mseto

Manufaa ya Handisheki: Kisumu kupata miradi ya Sh50 bilioni

August 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MRATIBU wa utekelezaji miradi ya serikali, Dkt Fred Matiang’i ametangaza kuwa Kaunti ya Kisumu itapokezwa na serikali kuu kitita cha Sh50 bilioni za miradi ya maendeleo katika mwaka 2019/20.

Eneo la Nyanza limekuwa likimulikwa kwa maendeleo mengi tangu kinara wa upinzani Raila Odinga asalimiane na Rais Uhuru Kenyatta na kuwa mmoja wa viungo thabiti kwa utawala wa Jubilee ambapo amezima kabisa harakati za kupinga serikali kwa lolote lile.

Akiongea Jumatano katika eneo la Migori, Dkt Matiang’i alisema miradi hiyo itakuwa njia moja ya kuharakisha maendeleo eneo hilo baada ya miaka ya kutelekezwa ambapo siasa za upinzani eneo hilo zilitajwa.

“Mradi wa kwanza utakuwa wa kujenga nyumba za makazi kwa walio katika pato la wastani na duni. Ujenzi huo ukishakamilika, nyumba zitauziwa wafanyakazi wa umma kwa bei rahisi ili kuwajenga katika maisha yao na hivyo basi kuwapa motisha ya kuendelea kuchapa kazi kwa roho safi wakiwa na uhakika wa kustaafu katika mazingira ya ustaarabu,” akasema Matiang’i.

Dkt Matiang’i alifafanua kuwa mradi huo unaoendeshwa kwa awamu kadha kote nchini unashirikishwa na mpango wa kisera wa Civil Servants Tenant Purchase Housing Scheme.

“Mradi wa Kisumu utatimizwa kwa kujengwa kwa nyumba 250 katika uwanja wa hekari 2.85 na ambao unakadiriwa kumalizika mwaka wa 2021,” akasema.

Alisema kuwa mradi huo utaimarisha sura ya eneo hilo kwa kuwa nyumba zote zitakuwa za ghorofa tano huku miundombinu katika mazingira yake ikiimarishwa.

“Tutaunda barabara, tuweke mitambo ya maji na kisha tuwatengenezee soko na eneo la burudani ndani ya mtaa huo mpya. Pia, nafasi ya kuegesha magari itakuwa pana na ya kuvutia,” akasema.

Yakikamilika, wafanyakazi wa umma watakaonufaika watazilipia kwa njia za mikopo ya polepole ambapo muda wa malipo umewekwa kuwa miaka 25.

Usalama

Waziri huyo anayewajibikia usalama wa ndani kwa sasa alisema kuwa kitita kingine ili kujumuisha Sh5 bilioni kitatumika katika ujenzi na ukarabati wa barabara za kaunti hiyo.

“Pia tutatumia pesa zingine katika uimarishaji wa utupaji majitaka, kuweka taa katika barabara za kaunti hiyo na pia kudhibiti maeneo hatari ya mafuriko,” akasema.

Mitaa ambayo itapewa kipaumbele ni Bandani, Manyatta Arabs, Nyalenda na Obunga ambapo ukarabati kuboresha mitaa ya mabanda utagharimu kitita cha Sh1.2 bilioni.

Alisema mradi huo wa uimarishaji mitaa duni utashirikishwa chini ya ufadhili wa pamoja wa serikali na Benki ya Dunia (WB).

Aidha, shirika la ujenzi wa nyumba la kiserikali (NHC) litazindua mradi wa kujenga 700 katika eneo Kanyakwar, zote kwa gharama ya Sh2.6 bilioni na pia mradi mwingine wa kutoa hatimiliki za mashamba uzinduliwe.