• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Watu aina saba watakaokuwa katika kivuli cha Mola siku ya kiyama

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Watu aina saba watakaokuwa katika kivuli cha Mola siku ya kiyama

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Subuhaanahu Wataala, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam. Leo tutaangazia watu saba watakaokuwa katika kivuli cha Allah siku ya Qiyaamah! Hakutakuwa na kivuli chochote ila kivuli chake Mwenyezi Mungu Azza wajalla.

Wa kwanza, ni “Kiongozi Muadilifu…”

Kutekeleza sheria kwa haki na uadilifu ni muhimu sana kwa mtawala yoyote, madhali yeye ndiye mshika hatamu wa watu wake na yeye ndio mtoa haki wa mwisho katika sehemu husika.

Kwa sababu hii, mtawala amepewa nafasi muhimu sana kama mmoja katika watu saba ambao watatunikiwa kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) siku ya Qiyaamah.

Wa pili, ni “Kijana aliyekulia katika kumcha Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)…”

Ni baraka iliyoje kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kijana ambaye ameongozwa kwenye ibada na akawa na urafiki au uongozo mzuri kwenye mambo mema, kwani kama tunavojua kuwa ni katika ujana wa mtu ambapo hukabiliwa na vishawishi vya dunia na huwa rahisi kuteleza kwenye njia ya Uislamu.

Hii inakuwa dhihirifu pale tunapoona kwenye jamii zetu na tunaona hadaa nyingi za kidunia, kama muziki, michezo, vilabu mbali mbali visiyvo vya kheri, mambo ya fasheni na kadhalika.

Hivi vyote huwa vimelenga au mlengwa mkuu katika mambo hayo tuliyoyataja hapo juu ni vijana.

“Ujana huwa mara moja tu na ujana ni moshi!” huwa wanaambiwa.

Wa tatu, ni “Mwislamu ambae moyo wake umesehelea (umeambatana) katika msikiti.…”

Kuna msisitizo mkubwa katika Sunnah kwa Muislamu mwanaume kuswali msikitini na malipo yake ni makubwa mno. Sio tu inamwezesha mtu astahiki kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) siku ya Qiyaamah, bali pia “…kila hatua anayochukua kuelekea msikitini hunyanyuliwa daraja moja na hufutiwa dhambi moja.

Wakati akiswali, Malaika hawaachi kumuombea madhali yuko katika sehemu ya ibada na husema, Ewe Allah mwingi wa rehema mrehemu mja wako huyu, Ewe Allah mwingi wa rehema mhurumie mja wako huyu…” [Al-Bukhaariy]

Wa nne, ni “Watu wawili wapendanao kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), wakakutana kwa ajili ya Mola wao na wakatengana kwa ajili ya Mola wao…”

Kuwa na upendo wa dhati kwa jili ya Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni moja ya milango mitukufu kuelekea kwenye mazuri ya huko akhera na ni chanzo cha kuonja uzuri wa Imani katika dunia hii. Kupendana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) inamaanisha Muislamu anatakiwa ampende Muislamu mwenzake kwa ajili ya usahihi au uongofu wa Dini yake. Bila ya kujali rangi, mtazamo wa kisura, anavaa nini,kama ni tajiri au maskini, anatoka wapi, au pengine ukachukia kila kitu chake ila ukampenda kwa ajili ya Imani yake: Huku ndiko kupendana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

Wa tano, ni “Mwanaume anayeitwa na mwanamke mrembo kwa kutaka kufanya matendo ya haramu na akasema “La hakika mimi namuogopa Allah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)…”

Dunia hii imejaa vishawishi ambavyo vinaelekeza kwenye moto wa jahanamu na miongoni mwa hivyo vishawishi ni vile vinavotokana na wanawake.

Wanaume wengi wameelekeza mioyo na nafsi zao kwenye maangamizi ya vishawishi vya wanawake na pia ndio maana Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuonya Ummah wake mahsusi kuhusu suala hili. Akasema, “Dunia ni nzuri na ya kijani na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atakuwekeni na Atakufanyeni nyinyi kuwa mlioendelea ili Aone mutakayoyatenda. Basi Jiepusheni na ushawishi unaotokana na wanawake: Hakika mtihani wa mwanzo wa wana wa Israaiyl ulisababishwa na wanawake.” [Muslim]

Wa sita ni “Mtu anayetoa sadaka kwa mkono wa kulia na wa kushoto usijue kitu kilichotendeka (atoae sadaka kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa siri bila ya wengine kujua …” Hii inaeleza aina ya mtu anayeelekea katika umbali wa hali ya juu kabisa katika kujilinda na kujiepusha na Riyaa (kufanya amali njema ili watu wamuone na kumsifu). Dhambi hii kubwa inaangamiza faida ambazo zimo kwenye amali njema na husababisha adhabu kali kwa yule anayefanya jambo hilo. Ni hatari kwa kuwa ni tabia ya binaadamu kupenda na kufurahia watu wakimhimidi (wakimtukuza).

Hivvo ni lazima tuwe makini sana na kuhakikisha kuwa nia zetu zinaanza na kuendelea kubakia kuwa safi kila mara tufanyapo amali njema kama kutoa sadaka. Si kama tunavoona leo ambapo katika Misikiti yetu utakuta watu katika kipaza sauti na mabao ya matangazo yanayosema, ‘Fulani katoa kadhaa kumpa Fulani kwa sababu kadhaa wa kadhaa!

Wa saba ni “Mtu anayemkumbuka Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa faragha na huku macho yake yakatokwa na machozi.” Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametueleza: “Ingelikuwa unayajua ninayoyajua mimi, ungeli cheka kidogo na ukalia sana.” [Al-Bukhaariy]

You can share this post!

Wakazi Gatundu Kaskazini wahakikishiwa fidia yao ya bwawa...

Anne Thumbi atoa masharti kabla mazishi ya Ken Okoth

adminleo