Makala

KIPWANI: Katia makali kijijini ila sasa awika mjini

August 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KIPAJI chake kiligunduliwa akiwa bado anaishi kijijini na sasa Ahmad Masoud Juma al-maarufu Qari Ibnu Masoud ni mmoja kati ya wanaoshamiri katika kuimba Qasida kutoka kundi la waimbaji wa nyimbo za dini ya Kiislamu cha SAS Angham.

Qari anasema alikuwa mwimbaji wa Qasida na msomaji wa Kuran kwa mahadhi (tajwidi) katika kijiji chao kule Mambrui, Kaunti ya Kilifi produsa Awadh Salim al-maarufu Shirko alipomjia mwaka 2010 na kumshawishi kuhamia Mombasa kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake.

“Tangu mwaka wa 2011, nimeweza kufanya kolabo za video na audio kadhaa za Qasida na wenzangu wawili, Shirko na Saad Faraj bali na kutoa Qasida zangu binafsi ambazo nashukuru zinaitikiwa vizuri na wapenda muziki,” akasema Qari.

Ulianza kuimba Qasida na kusoma Kuran kwa mahadhi lini?

Qari: Nilianza kuimba Qasida na tajwidi tangu nilipokuwa na umri wa miaka sita katika Madrassa.

Lipi lilisukuma kumfuata Shirko hadi Mombasa?

Qari: Niliamini Shirko ataweza kuinua kipaji changu. Na nilikubali kwenda kuishi Mombasa kwa kutambua hadhira hiyo ni kubwa ikilinganishwa na kule kwetu kijijini hivyo kunipa nafasi ya kazi zangu kusikilizwa na kusambazwa.

Qasida yako ya kwanza ilitoka lini ?

Qari: Qasida yangu ya kwanza ilikuwa ni Mzuri sana Nabia ambayo niliizindua 2012 na imetizamwa mara 190,000 katika YouTube.

Unatumia lugha gani na ni Qasida gani iliyokupatia umaarufu zaidi?

Qari: Natumia Kiswahili asilia cha Pwani na Qasida ya Kipenzi cha Yatima ndio ilinipa umaarufu zaidi kwani ilitumiwa kwenye stesheni za redio katika kampeni zao za kuwasaidia mayatima.

Hivi sasa una Qasida ngapi kwenye YouTube?

Qari: Zaidi ya Qasida 20 na kati ya zile zilizo maarufu ni Radhi za Wazazi, Nguvu za Mola, Tumswalie Karima, Anayo Alama, Ya Rasullallah, Nyoyo Zimefurahika, Siku tukufu ya Idd na Baba.

Umekuwa ukiangazia mambo gani hasa katika Qasida zako?

Qari: Nazugumzia mada mbalimbali kuhusu maisha ya kila siku nikiwataka waja kuishi kwa msingi wa dini na pia kuwasaidia mayatima na walemavu.

Mnaazimia kufika wapi na kikundi chenu cha SAS Angham?

Qari: Kufikia kiwango cha waimbaji maarufu Maher Zein na Sami Yusuf.

Unawaambia nini mashabiki wako?

Qari: Nawaomba wazidi kuniunga mkono kwani umaarufu wangu umetokana na kutambua kuwa wako na mimi wakati wote.