Michezo

TOSHA GARI! Tetesi zadai Manchester United yatafuta huduma za beki Maguire

August 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

TETESI zinadai kuwa Manchester United imewasilisha ofa rasmi ya Sh9.9 bilioni kutafuta huduma za beki wa Leicester, Harry Maguire.

Habari hizo ziliibuka siku ya Alhamisi zikisema kuwa “mashetani wekundu” United wameweka fedha hizo mezani na kuambia waajiri wake Leicester wakubali fedha hizo ama waziache kwa sababu hiyo ndiyo bei yao ya mwisho. Inasemekana kuwa United imetoa makataa ya Jumatatu ambapo itaondoa ofa hiyo iwapo Leicester haitakuwa imeikubali kufikia wakati huo.

Maguire amekuwa akitafutwa na United katika kipindi hiki chote cha uhamisho, na hatimaye mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wameamua kuonyesha tena kwamba wanamtaka ikisalia chini ya wiki moja kabla ya uhamisho kufungwa kwa klabu zinazoshiriki EPL.

Ikiwa uhamisho wa Maguire utakamilika, ada ya Sh9.9 bilioni itamfanya kuwa beki ghali duniani katika soka akimpiku Virgil van Dijk aliyesajiliwa na Liverpool kwa Sh9.3 bilioni kutoka Southampton mwaka 2018.

Habari za United kuomba rasmi huduma za Maguire zinawasili muda mfupi baada ya mchezaji huyo Mwingereza kuachwa nje ya video iliyopeperushwa kwenye ukurasa wa mtandao wa Twitter wa Leicester iliyofichua nambari za jezi za wachezaji wa wafalme hao wa EPL msimu 2015-2016 ambazo watavalia msimu 2019-2020.

Ingawa alithibitishwa kwenye tovuti ya klabu hiyo kuwa atavalia jezi nambari 15 katika msimu mpya, kukosekana kwake kwenye video hiyo kumeibua maswali. United inatumai itanyakua Maguire kabla ya kipindi kirefu cha uhamisho kutamatika Agosti 8.

Klabu hii inayonolewa na kocha kutoka Norway, Ole Gunnar Solskjaer pia inamezea mate Paulo Dybala na inatarajia kusajili mshambuliaji huyu wa Juventus kabla ya kipindi cha uhamisho kufungwa.

Ubadilishanaji

Usajili wa Dybala utashuhudia mshambuliaji Romelu Lukaku akielekea jijini Turin, ingawa ubadilishanaji huu unategemea pakubwa Dybala kukubali kuondoka Juve na kufanya Old Trafford kuwa makao yake mapya.

Ripoti zilifichua mnamo siku ya Jumatano kuwa raia huyo wa Argentina anataka mshahara wa zaidi ya Sh1.1 bilioni kila mwaka kabla ya kujiunga na United kwani hatua hiyo itamnyima soka ya Klabu Bingwa Ulaya msimu 2019-2020.

United inatumai kufanya Dybala na Maguire kuwa sajili wao wa tatu na nne mtawalia katika kipindi hiki cha uhamisho baada ya kunyakua winga wa Wales Daniel James na beki Mwingereza Aaron Wan-Bissaka.

Miamba hawa United wamekuwa na kipindi kizuri cha kujiandaa kwa msimu mpya chini ya Solskjaer. Wameshinda mechi zao zote tano. Vijana wa Solskjaer watakamilisha mechi za kujipima nguvu dhidi ya AC Milan leo kabla ya kuanza ligi kwa kualika Chelsea mnamo Agosti 11.