FUNGUKA: 'Mara moja tu, naitupa'
Na PAULINE ONGAJI
KWA wengi na hasa mabinti, usafi wa chupi ni muhimu sana.
Kulingana na viwango vya kawaida unapaswa kubadilisha chupi angalau mara moja kwa siku.
Hata hivyo, mambo ni tofauti kabisa kwa Bi Veronica ambaye usafi wake ameupeleka katika viwango vya kipekee.
Mrembo huyu ambaye ni daktari katika mojawapo ya hospitali za kibinafsi zinazotambulika nchini, anasema kila anapobadilisha vazi hili yeye hulitupa.
“Siwezi valia chupi zaidi ya mara moja. Kila ninapoivaa na kuivua, mimi huitupa. Sababu kuu ni masuala ya usalama wa afya. Naamini kwamba sehemu nyeti huwa na bakteria kibao hasa baada ya uchafu na jasho la siku nzima. Bakteria hizo zaweza kuniletea maambukizi iwapo nitasafisha kwa kawaida na kuvaa chupi ile tena.
Pia, sababu yangu ya kufanya hivyo ni usafi. Kila mara napenda kuhisi safi. Naamini kwamba uchafu mwingi unaojirundika katika sehemu hii waweza kusababisha maambukizi na harufu mbaya.
Aidha, tokea zamani mamangu alinifunza kwamba ni ishara ya uchafu kurudia chupi hata baada ya kusafisha. Chupi ni vazi la kuvaliwa mara moja na kutupwa.
Kunao wanaodhani kwamba tabia hii ni kutokana na uzito wa mfuko wangu. Na kusema kweli hawakosei. Hii bwana haitaki mfuko mwepesi. Mimi ni mmojawapo wa madaktari wanaoheshimika katika mojawapo ya hospitali zinazotambulika nchini.
Kuwa daktari tena anayeheshimika, bila shaka kunanihakikishia mshahara mzuri kumaanisha kwamba pesa kwangu sio tatizo. Hakuna chupi yangu ninayoinunua chini ya Sh1,500. Kwanza ile ninayovalia wakati wa kulala, inauzwa Sh1,500 dukani. Chupi zangu hasa huagizwa kutoka ng’ambo.
Nimetenga asilimia fulani ya mshahara wangu kugharimia ununuzi wa chupi pekee. Hata binti yangu nimeanza kumfunza haya kwani hata yeye akibadilisha chupi haisafishwi na kurudiwa, inatupwa.
Sio hayo tu. Hata ukiwa mpenzi wangu, lazima uwe tayari kubadilisha boksa/ngotha na kuzitupa kila siku, la sivyo hakuna uwezekano wetu kuwa pamoja. Ikiwa hauwezi kumudu haya maisha, niko tayari kukufadhili, la sivyo ushike hamsini zako.
Ni tabia ambayo ningependa iigwe na watu wengine sio tu kama mbinu ya kukabiliana na maambukizi yanayotokana na uchafu wa sehemu za nyeti, bali pia kama njia ya kudumisha usafi wa mwili”.