Makala

MWANASIASA NGANGARI: Waiyaki: Mwanadiplomasia na mwandani wa Kenyatta

August 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na KENYA YEAR BOOK

DKT Munyua Waiyaki ambaye alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia kabla na baada ya uhuru, anakumbuka miaka ya nyuma kwa fahari kuu, japo uzee unaendelea kumlemea, mvi kichwani na uso uliojaa makunyanzi.

Katika kipindi cha miaka 24 alizohudumu kwenye siasa, Dkt Waiyaki alikuwa nguzo muhimu kwenye utawala wa Rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta ambaye alikuwa rafiki wake wa dhati.

Vilevile alihudumu kwa kifupi kwenye utawala wa Rais Daniel Arap Moi kando na kuwa na uhusiano mzuri na makamu wa Rais wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga na Tom Mboya.

Mkongwe huyu ambaye pia ni msomi wa masuala ya utabibu alizaliwa katika kijiji cha Kiawariua, Muthiga, Kikuyu, wazazi wake wakiwa Tirus Waiyaki na Elizabeth Wairimu.

Bi Wairimu ambaye bado yu hai ana miaka 120 huku babake akikumbukwa kama Inspekta wa kwanza wa polisi Mwaafrika kusimamia kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.

Alizaliwa mwaka 1926 na kujiunga na shule ya upili ya Alliance 1942, ambapo alisoma pamoja na watu wengine walioibuka viongozi mashuhuri baadaye kama Paul Ngei, Jean-Marie Seroney, Mbiti Mate na Kyale Mwendwa.

Baada ya kuondoka Alliance, alijiunga na taasisi ya Adams, Natal nchini Afrika Kusini kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare ambako alikutana tena na Kyale Mwendwa, Mbiti Mate pamoja na Kasisi Chrispus Kiongo na waziri wa zamani Njoroge Mungai.

Ingawa hivyo, safari yake ya masomo iliyofuatia jijini London na Chuo Kikuu cha St Andrews nchini Scotland ilijaa vikwazo vingi darasani na nje kutokana na jinsi Wazungu walivyokuwa wakiwabagua Waafrika.

Alijitahidi na kwenye masomo hayo akiwa na baadhi ya viongozi waliorejea nchini na kuzua upinzani mkali dhidi ya serikali ya mbeberu kisha kufaulisha ndoto ya Kenya kujinyakulia uhuru.

Alirejea Kenya 1958 baada ya kusomea udaktari kwenye mataifa hayo ya uzunguni na akapata kazi ya daktari mtaalamu mpasuaji katika hospitali ya Machakos.

Mwaka moja baadaye, aliacha kazi ya serikali na akaanza kliniki yake katika jengo moja kwenye barabara ya Tom Mboya, Nairobi.

Alijiunga rasmi na siasa mwaka 1959 na kutagusana na watu watajika kama Charles Njonjo, Jaramogi Oginga Odinga, Tom Mboya, Daniel Arap Moi, Mbiyu Koinange na wengine wengi.

Kabla ya Mzee Jomo Kenyatta kuachiliwa kutoka gerezani 1961, Dkt Waiyaki alikuwa kati ya viongozi chipukizi waliomrai atumie chama cha Kanu kuwania uongozi wa nchi.

Kenya ilipojinyakulia uhuru mwaka 1963, Dkt Waiyaki alichaguliwa mbunge wa Nairobi Kaskazini-Mashariki kupitia tiketi ya chama cha Kanu.

Dkt Waiyaki ambaye alikuwa mkwewe Mzee Kenyatta (Mama Ngina ni wa ukoo wa mamake) aliteuliwa Waziri Msaidizi. Alishinda kiti hicho kwenye chaguzi za 1969, 1974 na 1979.

Eneobunge hilo lilibadilishwa jina na kuitwa Mathare kabla ya kubadilishwa tena 1997 na kuitwaa Kasarani.

Mwanasiasa huyo msomi alimtembelea Mzee Kenyatta nyumbani kwake Gatundu kila mara.

“Nilikuwa na uhusiano imara na Mzee Kenyatta na nilikaribishwa kwake kila mara. Wakati nilipokuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni, aliniruhusu niandamane na mke wangu kwenye ziara kadhaa za serikali nje ya nchi,” alisema Dkt Waiyaki.

Ingawa alitofautiana na Mzee Kenyatta, uhasama kati ya Dkt Odinga na Bw Mboya ulipotokota mnamo 1966, Bw Waiyaki alirejesha uhusiano huo na kwa usaidizi wa Bw Njonjo yeye pamoja na Fred Mati walichaguliwa Naibu Spika na Spika mtawalia.

Kabla ya kupokezwa wadhifa wa Naibu Spika, kiongozi huyo alihudumu kwenye kamati iliyokuwa ikishughulikia maslahi ya wabunge na hata wakati moja alipongezwa kwa kuhakikisha wabunge wanakula mlo uliopikwa vizuri kwenye mikahawa ya bunge.

Akihudumu kama Naibu Spika, hatasahau milele siku alipongoza vikao na aliyekuwa mbunge wa Butere Martin Shikuku alipotangaza hadharani kwamba Kanu imekufa na hata kutishia kupanda mgomba wa ndizi kwenye kaburi la Mzee Kenyatta.

Wakati wa vikao hivyo, mbunge wa Tinderet enzi hizo Jean Seroney ambaye pia alikuwa kwenye jopo la wasaidizi wa spika alikubaliana na matamshi ya Bw Shikuku hali ambayo ilimweka pabaya zaidi Dkt Waiyaki ikizingatiwa alikuwa akiunga mkono serikali.

“Sikushangazwa na matamshi ya Bw Shikuku ila nilimkosoa na kumwaamrisha awe na nidhamu bungeni. Kwa hasira, Bw Koinange aliondoka bungeni na ilikuwa dhahiri kwamba Mabw Shikuku na Seroney walipoondoka bungeni, walizuiliwa na kupelekwa kwenye jela,” akasimulia Dkt Waiyaki kuhusu mihemko ya kisiasa miaka ya 70.

Aidha anamkumbuka Mzee Kenyatta kama Rais asiyekubali mzaha na hakuna aliyedhubutu kubatilisha uamuzi wake ingawa alichukua uamuzi baada ya kushauriana na viongozi wenzake.

Mzee alipofariki, Dkt Waiyaki ambaye bado alikuwa Waziri wa masuala ya nchi za Kigeni alikuwa mjini Mombasa akiongoza mkutano wa kila mwaka wa mabalozi wa Kenya.

Alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliotazama mwili wa Mzee Kenyatta alipoaga dunia baada ya kufahamishwa habari hizo za mauti na mwanawe Rais, Peter Muigai saa tisa asubuhi na akatakiwa afike Ikulu kwa dharura.

Rais Mstaafu Daniel Arap Moi alipochukua hatamu za uongozi 1978, alimhamisha Dkt Waiyaki kutoka wizara yake ambayo ilikuwa ya hadhi na huo ukawa mwanzo wa kuporomoka kwa taaluma ya siasa ya kiongozi huyo.

Alistaafu siasa mwaka wa 1983 baada ya kushindwa kuhifadhi kiti cha ubunge cha Mathare kwenye uchaguzi mkuu, kiti ambacho Andrew Ngumba alikishinda na hatimaye kuwakilisha wakazi wake kwenye bunge la kitaifa.

Dkt Waiyaki ambaye siku hizi hutumia muda wake mwingi akifuatilia ujenzi wa nyumba zake za kukodisha na kuwachunga ng’ombe na kondoo kwenye shamba lake, alifiwa na mkewe kutokana na maradhi ya saratani miaka michache iliyopita.

“Huwa nafurahia kuwaona mifugo yangu kwenye shamba langu. Mwaka wa 2003 mke wangu alipatikana na maradhi ya saratani. Alifanyiwa upasuaji na tukaridhika kwamba ugonjwa huo umedhibitiwa lakini ulienea hadi kwenye figo majuma matatu baadaye,” akasema Dkt Waiyaki huku akimkumbuka mkewe kama aliyechangia kung’aa kwake kwenye siasa miaka ya 60 na 70.

Muumini kindakindaki

Kiongozi huyo wa zamani ambaye anamiliki taasisi ya mafunzo ya Global, mtaani Muthiga pia ni muumini kindakindaki wa kanisa la PCEA na kila Jumapili hushiriki kwenye kanisa la Kihumo.

“Ingawa nilitoa ardhi ambayo kanisa la PCEA Loresho lilijengwa, huwa nahudhuria ibada katika lile la zamani la Kihumo,” akasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe mara nyingi hushiriki vikao na wazee wenzake na wageni wanaomtembelea nyumbani mwake huku akiwa msomaji mahiri wa majarida na vitabu vya kidini vinavyotoa ufafanuzi wa ndani na kina kuhusu mafungu mbalimbali ya bibilia.