Makala

KINAYA: Vipawa vya siasa vimezidi nchini, sijui mbegu zake zihifadhiwe wapi

August 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

UNATAKA kuniambia Kenya tunazalisha vipawa vingi kuliko tunavyohitaji? Vipi tena? Hebu angalia kwenye ulingo wa siasa uniambie tutawapeleka wapi watu hao.

Vita vingi vinavyoendelea kwenye kaunti mbalimbali nchini vinatokana na wingi wa vipawa, ndio maana nasalitika kuuliza: tumebarikiwa, au tumelaaniwa?

Kaunti ya Nairobi pekee tuna vigogo wa siasa ambao wanatarajiwa kuwania cheo kimoja, ila ni mmoja pekee atakayekitwaa.

Gavana Sonko na Seneta Sakaja wanataka kulana maini kwa visingizio, lakini tunajua kisa na mkasa ni kinyang’anyiro cha ugavana cha 2022.

Wanaonekana kumsahau aliyekuwa gavana, Evans Kidero, tajiri wa kutupwa ambaye, japo tunamsikia mara moja moja kwenye mizani ya haki, tunajua atazichapa nao.

Ukiangalia Mombasa, unatambua ‘Sultan Mwitu’ anastaafu ugavana ifikapo 2022. Atakwenda wapi? Hoja si atakakokwenda bali atakayemrithi.

Wanaokimezea mate kiti hicho ni bwanyenye Suleiman Shahbal na Hassan mwana wa Sarai, kila mmoja akitamani kukikalia kwa makalio yote mawili kwa miaka 10.

Ukiwauliza Shahbal na Hassan, ni mmoja kati yao atakayekipata. Lakini vyao ni vita vya panzi wawili vinavyoweza kuishia kwao kuliwa na kunguru.

Ala! Kunguru ni nani hapa? Usiniambie umemsahau ‘Bwana Usafi’ anayetangamana na watalii siku hizi – Najib Balala.

Kumbuka mbunge huyo wa zamani wa Mvita aliwania ugavana wa Mombasa ila akabwagwa na ‘Sultan Mwitu’ mnamo 2013, akapata afueni kwa kuteuliwa waziri.

Aliyemteua ataondoka Ikulu na kuelekea nyumbani na hatuna hakika mrithi wake ni nani, hivyo ‘Bwana Usafi’ hawezi kuketi chini ya mnazi akisubiri nazi zianguke apate mlo.

Usishtuke Shahbal na mwana wa Sarai wakipigana wachoke na kutazamana kama majogoo, ‘Bwana Usafi’ awafanye kitoweo chake.

Je, mbona Wakenya wamedanganyika kwamba Gavana wa Kirinyaga, Ann Waiguru, na mbunge wa kike, Purity Wangui Ngirici, ndio pekee watakaozichapa hatimaye?

Naye Malkia wa Gichugu, Martha Wangari Karua, ambaye hutema cheche za moto kila akipanua kinywa? Siasa zake haziendani na za mlimani. Zilipendwa! Hatishi. Labda.

Mambo yatabadilika iwapo atatua huko mbunge wa zamani wa Ndia, Robinson Njeru Githae, ambaye sasa ni balozi wa Kenya nchini Austria.

Githae, mwanasiasa mzito, ni mmoja wa wanaotarajiwa kuwa mayatima wa kisiasa wa mwenyeji wa sasa wa Ikulu, hivyo huenda akajitosa ulingoni!

Ukikutana na Waiguru na Ngirici waambie wasizozane sana wakamsahau adui aliye nje lau sivyo kila mmoja achomwe mkuki na kwenda kuuguzia majeraha kijijini kwao.

Toka Kirinyaga uteremke hadi Kaunti ya Meru, uwapate Gavana Kiraitu Murungi na Seneta Mithika Linturi wakipakana matope hadharani kabla ya kipenga kupulizwa.

Wasiloonekana kukumbuka ni kwamba mtangulizi wa Bw Kiraitu, Peter Gatirau Munya, angali huku na sasa ana ushawishi wa hali ya juu wa mamlaka na mafedha.

Munya ndiye waziri wa biashara na viwanda, kwa hivyo ana uwezo wa kutandaza noti mpya za Sh1000 kote Meru na kuwazika wawili hao wakiwa hai.

Tutafuteni kwa kuyafungia mabaki ya wanasiasa ili tuhifadhi mbegu zao. Si kuzaliana kwema hutokana na uhifadhi na utunzaji bora wa mbegu.

 

[email protected]