• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
DINI: Anayenyenyekea hukwezwa ilhali yule anayejikweza hunyenyekezwa

DINI: Anayenyenyekea hukwezwa ilhali yule anayejikweza hunyenyekezwa

Na FAUSTIN KAMUGISHA

UNYENYEKEVU ni mtihani.

Unapojivuna kuwa umeupata unyenyekevu unapotea. Kama wewe ni mnyenyekevu usiwaambie watu kuwa wewe ni mnyenyekevu.

“Kuanguka hakuumizi wale ambao wanapaa chinichini” (Methali ya China). Ukipaa juu sana unapoanguka unaumia sana. Wanyenyekevu wanapaa chinichini.”

Yeyote yule ajikwezaye mwenyewe atanyenyekezwa, na yeyote yule ajinyenyekezaye mwenyewe atakwezwa.” Ukijishusha, utapandishwa.

Unyenyekevu na kujiamini ni pande mbili za sarafu moja.

Kwangu mimi unyenyekevu na kujiamini ni kama mkono wa kushoto na mkono wa kulia. Unahitaji mikono yote miwili kushikilia mafanikio. James Alberione (1884-1971) mzaliwa wa Italia na mwandishi alilinganisha unyenyekevu na mguu wa kushoto na kujiamini na mguu wa kulia, alisema,

“Katika unyenyekevu na kujiamini tusonge mbele bila pozi. Unyenyekevu ni mguu wetu wa kushoto, kujiamini ni mguu wetu wa kulia. Tutumie miguu yote miwili ili kutembea vizuri.”

Msingi wa unyenyekevu na ubinadamu ni udongo. Maneno “humility” (unyenyekevu) na “human” (binadamu, na kibinadamu) yanatokana na neno la kilatini “humus” (udongo). Nyakati mbalimbali katika shughuli za kidini tunasikia maneno, “Wewe ni udongo na udongoni utarudi.”

Taswira ya udongo inabainisha masomo mengi. Kwanza udongo mikononi mwa mfinyanzi unatii. Sisi ni wafinyanzi pamoja na mfinyanzi Mkuu-Mwenyezi Mungu.

“Neno la kutia moyo kutoka kwa mwalimu kwa mtoto linaweza kubadili maisha. Neno la kutia moyo kutoka kwa mwenzi wa ndoa linaweza kuokoa ndoa. Neno la kutia moyo kutoka kwa kiongozi linaweza kumpatia mwanga mtu kufanya anachoweza kufanya,” alisema mtaalamu wa uongozi John C. Maxwell.

Mwalimu ni mfinyanzi wa wanafunzi. Mwanafunzi awe tayari kufinyangwa na mwalimu.

Wanandoa ni wafinyanzi wa ndoa yao, kama ndoa inavunjika au inadumu ni jambo ambalo liko mikononi mwao. Kiongozi ni mfinyanzi wa waongozwa.

Taswira ya udongo ni kubadili vitu vilivyooza na kuwa na uhai. Mbegu ikipandwa katika udongo na kuoza baadaye inachipuka na kuzaa sana. Ni katika unyenyekevu tunaweza kubadili uozo.

Pia udongo unatupiwa takataka, unakanyagwa laini mwisho wa siku mikungu ya ndizi inauinamia udongo, matunda yote yanatoa heshima kwa udongo. Ukinyenyekea utaheshimiwa. Nyenyekea ule vya watu na vya Mungu.

“Unyenyekevu ni jambo la kuomba kila mara uwe nalo na ukiwa nalo usimshukuru Mungu kuwa unalo,” alisema M.R. De Haan.

Unapoanza kumshukuru Mungu kuwa wewe ni mnyenyekevu unaingia kwenye uwanja wa majivuno.

Mwanasayansi Sir Isaac Newton baada ya kugundua kanuni za kisayansi alisema, “Sijui ninavyoonekana kwa dunia, lakini nijionavyo nimekuwa kama mvulana mdogo nikicheza kwenye ufukwe wa bahari nikishughulikia mambo mengine kitambo hiki na kitambo kile nikiona changarawe laini au gamba zuri zaidi lisilo la kawaida, wakati huo bahari kubwa ya ukweli ipo mbele yangu haijagunduliwa.”

Machache tu!

Kwa unyenyekevu mkubwa mwanasayansi huyo alimaanisha kuwa aliyoyagundua ni machache ukilinganisha na ambayo hatujui.

Katika uwanja wa elimu kadiri tunavyojua mengi tunagundua kuna mengi ambayo hatujui.

Unyenyekevu ni ufundi wa kujishusha na kuwa kama nukta. Nukta inaweza kubadili mambo.

Ukiwa na tarakimu hizi 5,000,000 kama ni pesa ukiweka nukta mbele ya sifuri sita unakuwa na shilingi tano. Ukiiweka mbele ya sifuri sita unakuwa na milioni tano.

Wewe ni nukta katika jamii, inategemea namna unavyoingia katika jamii na mtazamo hasi au chanya.

Mtu yeyote, akiingia na mtazamo chanya, na mtazamo wa kurithisha kizazi kijacho kitu kizuri, ataibadili jamii, ataiprogramu kupenda kusoma, kupendana, kupenda kazi na kuyapenda maendeleo na ustawi.

You can share this post!

Rais Kenyatta awataka viongozi kuiga mfano wa Laboso

Mzozo kuhusu Ken Okoth kurejea mahakamani

adminleo