Michezo

Ndoto ya Harambee Stars kushinda Afcon itatimia – Mashabiki mitaani

August 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

KATIKA dimba la AFCON 2019, Harambee Stars iliwekwa katika kundi ngumu lililojumuisha Algeria, Senegal na Tanzania.

Kilichofuata kinaeleweka vyema kwa kuwa baada ya kulemewa na Senegal na Algeria 2-0 na 3-0 mtawalia, Harambee Stars ilijinyanyua na kucharaza Taifa Stars ya Tanzania 3-2 na kurejea nyumbani kufuatilia dimba hilo.

Hata hivyo, kunao wanao ucheshi mwingi kama Carol Muthoni ambaye ni shabiki sugu wa Harambee stars na ambapo hufuatilia michuano katika mtaa wa Sabasaba, Kaunti ya Murang’a.

“Usiseme kuwa Harambee Stars ililemewa…Wanaojua kwa dhati kilichotendeka watakwambia kuwa Kenya ilimaliza katika nafasi ya tatu katika dimba hilo,” asema.

Anasema kuwa “ikiwa tulikuwa katika kundi moja na Senegal na Algeria na ambao waliishia kumenyana katika mchuano wa fainali, na tulikuwa katika kundi hilo pamoja na Tanzania na sisi tukamaliza michuano ya makundi tukiwa nambari tatu, ina maana kuwa ukitafsiri hili kwa kina na Kisayansi, jibu litaishia kuwa Harambee Stars ndiyo ilikuwa ya tatu bora katika Afcon 2019.”

Kwa usahihi wa utaratibu wa michunao ya Afcon 2019, timu ya Super Eagles ya Nigeria ndiyo iliibuka ya tatu baada ya kucharaza timu ya Tunisia.

Hata hivyo, katika ile hali ya ucheshi na hisia za ushabiki, Bi Muthoni ako na lake halali analosema hasa ukizingatia kuwa akitetea mrengo wake wa Harambee Stars, kila aina ya propaganda, upindaji haki na uvunjaji wa takwimu utaingia….na uishie kukumbatiwa kama ukweli na walio na maoni sawa na yake.

Hivyo, kuna michuano mingine ya Afcon 2021 ambayo imetolewa ratiba na ambapo Harambee Stars itamenyana na kisiwa cha Comoros, taifa la Togo na Misri.

Bi Muthoni anapiga nduru ya kivita, ingawa anakiri kuwa vita halisi ikitokea atasaidika na mguu wake akitoroka kwa kuwa anaichukia na kuiogopa, akisema kuwa “tutatinga bora zaidi kuwa katika Taifa la Cameroon ambalo litakuwa mwenyeji wa michuano hiyo.”

Matumaini tele

Anasema kuwa “tutaenda droo na Misiri ugenini kwao, hapa Kenya Kasarani tuwatandike na kisha tutandike Comoros na Togo katika kila awamu na tujipate Cameroon ambapo kabla ya lolote lingine, tutatembelea boma la Samuel Etoo kujulia hali wote wao wanaoishi hapo…”

Anasema kuwa amepewa motisha na hakikisho la rais wa Shirikisho la Kandanda Nchini Kenya (FKF) Nick Mwendwa ambaye “ametangaza kuwa itakuwa desturi kwa Kenya kuwa katika michuano ya Afcon.”

Mzawa wa 1979, akifahamika kama Nicholas Mwendwa Kithuku ambaye ni mume na pia baba kwa watoto wawili, ametangaza kuwa kuanzia Afcon 2019, Kenya itakuwa ikitinga kila awamu ya michuano hiyo na kulenga kubeba kombe hilo.

Mtaalamu huyu wa masuala ya kiteknolojia, sasa anasema kuwa “sio lazima iwe ni 2022 ambapo Harambee Stars itatua katika dimba la ulimwengu.”

Anasema kuwa “kabla niage dunia, kuna uwezekano kuwa tutatua katika uga wa kumenyana fainali za kombe la dunia na tuibuke kidedea tukibeba hilo kombe hadi hapa Kenya.”

Hilo ni sawa na kusema hana imani kuwa hilo linawezekana, lakini bora matumaini, maisha yanasonga.

Mwendwa ndiye mumiliki wa Klabu cha soka cha Ligi ya Kenya, Kariobangi Sharks na pia ni mwekezaji katika kampuni ya Riverbank Solutions Ltd.

Anasema kuwa uongozi wake hadi sasa umezua matunda mema kwa taifa hili ambapo timu ya wanawake ya soka imefanikiwa kujiunga na ushindani wa mabingwa barani Afrika kwa mara ya kwanza.

Pia, anasema kuwa ushirika wake na serikali umekuwa thabiti na pia amekuwa akishauriana na rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja kuhusu mbinu za kuinua viwango vya soka nchini.

Anasema kuwa afisi ya waziri wa Michezo imekuwa rafiki wa FKF na hatimaye kuna ule ushirika wa kufana kati ya FKF na serikali za Kaunti hasa katika safu ya kusukuma ujenzi wa viwanja nchini.

Mwenda anasema kuwa licha ya kuwa alirithi afisi iliyokuwa na madeni na kesi kadha kortini, ameweza kusukuma utenda kazi wa afisi hiyo hadi kutuliza mawimbi ya mali yake kupigwa mnada.

Anasema kuwa uongozi wake umezaa matunda katika kuimarisha Harambee Stars ambapo mkufunzi wa kimataifa Sebastien Migne, amechukua usukani wa Harambee Stars kinyume na hali za awali za kutegemea ukufunzi “wa kienyeji.”

Mwendwa anasema kuwa timu za walio chini ya miaka 13 na 17 kwa sasa zinajivunia mwamko mpya kupitia ufadhili.

Ndoto itatimia

Ni mikakati hiyo anasema kuwa itazua hali ya matumaini makuu kuwa Harambee Stars kufuzu na kuibuka washindi katika fainali za ulimwengu “ni ndoto ambayo ni halali na itatimia kabla niage dunia.”

Lakini anasema kuwa kwa sasa hana la kuaibika nalo kwa kuwa amekuwa muwazi na pia ameshirikisha elimu ya wakufunzi na wengine katika uratibu wa soka ili kuwapa makali ya kimataifa.

Lakini Bi Muthoni anasema kuwa “hayo ni sawa lakini kwanza tuondoe ukabila katika uundaji wa timu ya Harambee Stars kwa kuwa hakuna ukweli kuwa soka Kenya hii ni ya kabila moja kwa asilimia 90 na nyingine kwa asilimia tisa na wengine wote wakimenyania asilimia hiyo moja inayosalia.”

Anasema kuwa hilo lilijiangazia kwa uzito katika Afcon 2019 “na ambapo hata waliosihia kung’aa na kutusaidia pakubwa ni wale kutoka asilimia tisa, huku kukiwa na mmoja tu wa wale wa asilimia 90 ambaye alionekana kujielewa ugani.”

Ili kutinga fainali za Afcon 2021, anasema kuwa ni lazima hali hii ya ukabila katika kikosi iangamizwe.