• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Wito wa kumng’oa Trump wapata nguvu bungeni Amerika

Wito wa kumng’oa Trump wapata nguvu bungeni Amerika

NA MASHIRIKA

WITO kutaka Rais Donald Trump abanduliwe mamlakani umezidi kupata umaarufu bungeni, baada ya wanachama zaidi wa Democrats Ijumaa kujiunga na muungano unaosukuma hoja hiyo.

Ijumaa, zaidi ya wanachama 20 wa chama cha Democrats walitangaza kuunga mkono uchunguzi dhidi ya Trump, baada ya ushahidi uliotolewa na wakili wa serikali Robert Mueller, wiki iliyopita.

Msukumo huo umekuwa ukipata umaarufu tangu Mueller alipotoa ushahidi akisema kuwa Trump anaweza kushtakiwa kwa kukiuka sheria, akitoka afisini.

Mnamo Ijumaa, idadi ya wanachama wa Democrats wanaotaka Trump ang’atuliwe iliongezeka, hali ambayo imemzidishia presha spika wa bunge Nancy Pelosi kupitisha hoja hiyo, japo amekuwa akiipinga.

Wanachama 118 wa Democrats, kati ya idadi jumla ya 235 walitangaza kuwa wanaunga mkono uchunguzi uanzishwe dhidi ya Trump, kwa lengo la kumng’atua- kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la The Washington Post.

Ni wito ambao umezidi kupata nguvu, wakati wanaharakati nao wamekuwa wakilalamika kuwa baadhi ya maafisa wakuu serikalini wanakataa kumkabili Trump.

Mwanachama wa Democrat Salud Carbajal aliongeza idadi ya wanachama hao baada ya kutangaza Ijumaa kuwa hawataruhusu vitendo vya Trump kufumbiwa macho.

“Hatuwezi kupuuza vitendo vya Rais na hatutaruhusu akwepe kwa kuwa ni Rais,” Carbajal alisema katika ujumbe wake wa kutangaza kuunga mkono uchunguzi dhidi ya Trump.

Wakati wito huo ukizidi kupata umaarufu, Pelosi Ijumaa alitoa ujumbe ambao ulieleza kuhusu uchunguzi ambao bunge linaendeleza, japo hakutangaza ikiwa uchunguzi rasmi utaanzishwa kuhusu madai hayo.

“Nchini Amerika hakuna mtu aliye juu ya sheria. Rais atahitajika kujukumika kutokana na matendo yake,” Pelosi alisema, akiongeza kuwa wanachama wa Democratic wataendelea kutunga sheria na kuchunguza.

Wiki iliyopita, bunge lilituma maombi kortini, likitaka ushahidi uliotolewa katika ripoti ya Mueller, ili kubaini ikiwa liendelee kumchukulia Trump hatua katika bunge kikatiba, kama vile kumng’atua.

Mwenyekiti wa kamati ya mahakama bungeni Jerrold Nadler alisema kuwa kufikisha ombi hilo kortini ni sawa na kuanzisha uchunguzi dhidi ya Trump, kwa lengo la kumuondoa madarakani.

Trump na wengi wa maafisa wake wamekuwa wakidinda kutii miito ya bunge, hali ambayo imelazimu bunge kutafuta msaada kortini.

Ripoti ya Mueller ambayo ilitolewa mnamo Aprili ilisema kuwa kuna ushahidi kwamba Trump amevunja sheria kwa zaidi ya matukio kumi.

You can share this post!

Spika awashauri magavana kuandaa manaibu kuongoza

Afuta harusi kugundua baba mkwe ni mganga

adminleo