Jaji Ojwang' arejeshwa kazini
NA CHARLES WASONGA
JAJI wa Mahakama ya Juu Jacktone Ojwang’ sasa yu huru kurejelea majukumu yake baada ya jopo liliteuliwa kuchunguza makosa aliyodaiwa kuyatenda kutompata na hatia.
Alikuwa anakabiliwa na tuhuma za utendakazi mbaya, kutotenda haki na kukiuka kanuni za kuongoza utendakazi wa majaji.
Hata hivyo, wanachama wa jopo lililochunguza madai hayo, chini ya uongozi wa jaji wa mahakama ya rufaa Alnashir Visram ilimwondolea makosa baada ya kuchanganua ushahidi kutoka kwa zaidi ya mashahidi 15.
Jopo hilo liliwasilisha ripoti yake kwa Rais Uhuru Kenyatta Jumapili jioni na kupendekeza kuwa amri ya kumsimamisha kazi jaji Ojwang’ iondolewe na arejee kazini “mara moja.”
Vikao vya jopo hilo viliendeshwa faraghani.
Wale waliotoa ushahidi mbele ya jopo hilo ni pamoja na Jaji Mkuuu David Maraga. Taarifa ya Bw Maraga iliwasilishwa kwa niaba yake na Msajili wa Idara ya Mahakama Bi Anne Amadi.
Siku ya kwanza jopo hilo lilizuru Migori kubaini madai kuwa kuna barabara ya lami kuelekea nyumbani kwa Ojwang’ iliyojengwa na serikali ya kaunti hiyo.
Ilidaiwa kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulitekelezwa kama zawadi kwa Jaji Ojwang’ kutokana uamuzi wa kupendelea alioutoa kuhusiana na kesi moja iliyomkabili Gavana Okoth Obado.
Dai hilo liliwasilishwa kwa Tume ya Huduma ya Majaji (JSC) na Bw Nelson Onyango na watu wengine wanane na likajenga msingi ambapo tume hiyo ilitumia kupendekeza jaji huyo asimamishwe kazi.
Walalamishi hao walidai kuwa jaji huyo alishirikiana na majaji wengine wa Mahakama ya Juu kusikiza kesi iliyohusisha kaunti ya Migori, “ilhali ni mshirika wa karibu wa Gavana Obado kwa sababu gavana huyo aliweka lami barabara inayoelekea nyumbani kwa Ojwango.”
Kulingana na walalamishi hao Jaji Ojwang alipaswa kuarifu mahakama hiyo na wahusika wengine kuhusu uhusiano wa karibu uliopo kati yake na gavana Obado.
Ojwang alisimamishwa kazi baada ya JSC kutoa pendekezo kwa Rais Kenyatta kwamba abuni jopo la kuchunguza mienendo yake.
Rais Kenyatta aliunda jopo hilo mnamo Aprili 2. Lilijumuisha wanasheria wafuatao; Jaji (mstaafu) Festus Azangalala, Ambrose Weda, Andrew Bahati Mwamuye, Lucy Kambuni, Sylvia Wanjiku Muchiri na Amina Abdalla.
Mawakili Paul Nyamodi na Stella Munyi waliteuliwa kuwa wasaidizi wa jopo hilo.