• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Anatamba katika uigizaji licha ya kuzaliwa kwa uhawinde

Anatamba katika uigizaji licha ya kuzaliwa kwa uhawinde

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI hakuna kisichowezekana kwa kumwaminia Mungu maana maisha ya uchochole yalichangia haishi katika makao ya wasiojiweza ya Mama Teresa, maarufu Mji wa Huruma, Nairobi hadi alipotimiza umri wa miaka 21.

Katika makao hayo aliishi pamoja na dada zake wawili nao ndugu zake watatu waliishi katika familia za waMWtoto mayatima za Undugu Society na Kwetu Home of Peace.

Licha ya kupitia hayo, Esther Josephine Mueni anaamini nyota yake itang’aa zaidi na kuibuka kati ya waigizaji watajika duniani.

Dada huyu ni mwigizaji, prodyuza, mwandishi wa script, mpodozi pia anamiliki brandi ya kuzalisha filamu. ”Nilianza kujifunza masuala ya uigizaji kanisani tangu nikiwa mdogo nikisoma darasa la sita,” anasema.

Hayo tisa. Kumi kisura huyu amehitimu kwa shahada ya digrii kuhusu masuala ya fedha kwenye Chuo Kikuu cha St Pauls, Limuru. Hata hivyo ni taaluma inayoendelea kuyeyushwa na kipaji cha uigizaji. Katika uhusika wake anafahamika kwa majina mawili tofauti ikiwamo ‘Njoki’ pia ‘Kavindu.’

”Ninaamini nitafika mbali maana nakumbuka niliwahi kusafiri nchini Uchina nilikofanya kazi ya uigizaji ndani ya mwaka mmoja unusu,” alisema na kuongeza kuwa ni hatua iliyompa motisha zaidi.

Nchini Uchina akiwa na wenzake Wakenya wawili walikuwa wakiigiza sauti kwenye filamu ‘Doudou na Her Mothers’ iliyofanywa kwa lugha ya taifa hilo.

Msanii Esther Josephine Mueni. Picha/ John Kimwere

Pia ameshiriki vipindi kadhaa vilivyofanikiwa kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini. Msanii huyu anajivunia kushiriki kati ya vipindi maarufu nchini cha ‘Papa Shirandula’ ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya Citizen TV.

Aidha alikuwa kati ya walioshiriki kipindi cha ‘The Tussle’ kilichopeperushwa kupitia runinga ya KBC. Katika utangulizi wake alifanya kazi ya uigizaji na kundi la Simba Vision.

Chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu fupi ‘The Adjunct ‘ waliozalisha chuoni humo ambapo ndiye aliyoiandika. Baada ya kutamatisha masomo ya chuo kikuu mwaka 2014 amebahatika kufanya kazi ya kuzalisha filamu akiwa prodyuza chini ya Global Oak Media.

”Kando na uigizaji nimewahi kushiriki matangazo ya kibiashara ya Safaricom mara mbili. Najivunia kupiga hatua katika uigizaji ingawa mwanzoni nilipondwa na wengi wakidai siwezi kufanikiwa maana nilizaliwa katika familia maskini,” alisema.

Mwigizaji huyu ambaye ameolewa na kubarikiwa watoto watatu anadokeza kuwa anajiandaa kuzamia miradi kadhaa mwaka ujao. Kupitia brandi yake ”Smart Edge Media’ aliyoanzisha mwaka 2013 analenga kuzalisha filamu fupi zenye mafunzo pia zinazogusa jamii kwa jumla.

Katika uigizaji wake ingawa amekawia bila kushiriki filamu yoyote analenga kufuata nyayo zake staa wa maigizo mzawa wa Marekani

Taraji P Henson aliyejipatia umaarufu kutokana na filamu ya Empire.”

Veterani huyo pia ameshiriki filamu kama ‘What Men Want,’ ‘Tyler Perry’s Acrimony,’ ‘Hidden Figures,’ na ‘The Best of Enemies,’ kati ya zinginezo.

Kama prodyuza anatamani kufikia hadhi ya msanii tajiri duniani mzawa wa marekani Tyler Perry. Katika mpango mzima anataka kuzalisha filamu zitakaoibuka bora na kumpa umaarufu wa kukumbukwa miaka ijayo.

You can share this post!

Kahawa Queens wanusia ubingwa

Kinyago United yalipua State Rangers 7-1

adminleo