• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Usalama waimarishwa kwenye tamasha za muziki Kabarak

Usalama waimarishwa kwenye tamasha za muziki Kabarak

NA ANTHONY NJAGI

USALAMA umeimarishwa katika Chuo Kikuu cha Kabarak huku Tamasha za Kitaifa za Sanaa na Muziki, makala ya 93 zikiingia siku yake ya nne.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Nakuru Simon Matu alisema polisi kutoka vituo vya karibu na chuo hicho wametumwa kwenye maeneo kadhaa ambayo ni makazi ya muda kwa washiriki zaidi ya 130,000 katika tamasha hizo.

Bw Matu aliwahakikishia wenyeji na wageni katika hafla hizo kwamba anahusika na masuala ya usalama kibinafsi na atafanya juu chini kuwapa ulinzi wa kutosha.

“Nimeridhishwa kwamba kila kitu ki shwari tangu tamasha hizi zianze. Hakuna chochote kibaya ambacho kimetokea hadi kufikia sasa,” akasema Bw Matu.

Kamishna wa Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya naye aliwataka washiriki wote kushirikiana na maafisa wa usalama ambao wametumwa kwenye makazi yao ya muda ili kuzima utovu wowote wa usalama.

Akizungumzia tamasha hizo, Gavana Lee Kinyanjui alisema kuandaliwa kwa makala ya mwaka huu katika kaunti hiyo kutawapa wageni nafasi ya kufurahia mandhari na maeneo mengi ya kitalii.

Aidha, Bw Kinyanjui alifichua kwamba Serikali Kuu inashirikiana na utawala wake kuhakikisha kwamba tamasha hizo zinaendelea bila tatizo lolote hadi siku ya mwisho.

You can share this post!

Wasia wa mfu utakuwa ukizingatiwa utata ukiibuka –...

Korti kuamua Agosti 8 ikiwa Waititu ataendelea na kazi

adminleo