Habari

Ufunguo wa Ikulu 2022 unashikiliwa na Uhuru na Raila – Kamket

August 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

MBUNGE wa chama cha Kanu sasa anadai kuwa wanasiasa wanaopinga Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga watajipata katika upinzani baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbunge wa Tiaty William Kamket Jumanne alisema kuwa viongozi wawili hao ndio wanaoshikilia ufunguo wa Ikulu.

“Wakenya wenzangu, rais atakayeongoza nchi baada ya uchaguzi wa 2022 ataamuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga. Watu wanaopinga hilo watajipata katika upinzani,” akasema Bw Kamket.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Kiongozi wa Kanu Gideon Moi ambaye pia ni Seneta wa Baringo, amekuwa akidai kuwa chama cha Jubilee tayari kimesambaratika.

Bw Kamket ni miongoni mwa wanasiasa wachache ‘waasi’ kutoka ukanda wa Bonde la Ufa wanaopinga Naibu wa Rais William Ruto kuwa kuwania urais 2022.

Bw Moi ambaye ni mwanawe Rais wa Pili wa Kenya Daniel arap Moi, amekuwa akionyesha dalili za kutaka kuwania urais 2022 japo hajatangaza rasmi.

Viongozi wengine kutoka Bonde la Ufa wanaochukuliwa kuwa waasi ni wabunge Joshua Kutuny (Cherangany), Silas Teren (Moiben), Alfred Keter (Nandi Hills) na aliyekuwa mwaniaji wa ugavana katika kaunti ya Uasin Gishu Zedekiah Bundotich Kiprop (Buzeki).

Gavana wa zamani wa Bomet Isaac Rutto amekuwa vuguvugu na hajaonyesha dalili za kumuunga mkono Dkt Ruto au la.

Bw Kamket alionekana kuonya Dkt Ruto na wanasiasa wanaomuunga mkono, maarufu kundi la Tangatanga, ambao wamekuwa wakipinga handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kundi la Tangatanga wanashuku kuwa handisheki huenda ikawa mwiba kwa ndoto ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta atakayestaafu 2022.

Rais Kenyatta mwezi uliopita alisema kwamba: “atakayekuwa rais 2022 atachaguliwa na Mungu’.