• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uhuru ‘ajiuma ulimi’ akihutubu Jamaica

Uhuru ‘ajiuma ulimi’ akihutubu Jamaica

MASHIRIKA Na VALENTINE OBARA

Rais Uhuru Kenyatta Jumanne ‘alijiuma ulimi’ wakati alipokuwa akitoa hotuba kwenye ziara yake jijini Kingston, Jamaica.

Huku akieleza kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Kenya na Jamaica, Rais alinuia kueleza kwamba kuna hata vizazi vya Wajamaica humu nchini.

Katika harakati hizo, alichanganyikiwa na kuambia waliokuwemo ukumbini kuwa mama mkwe wake pia ni Mjamaica, ilhali hakumaanisha hivyo.

“Waziri Mkuu (wa Jamaica Andrew Holness) aliniambia jinsi makundi ya Wajamaica yamo katika karibu kila nchi humu duniani kwa hivyo alitaka kujua kama tunaweza kuwa nayo pia nchini Kenya. Nilimwambia ndio, naweza kuthibitisha kwa sababu hata ‘mamake kaka ya mke wangu’ ni mwenye asili ya Jamaika,” akasema Rais.

Tamko hilo lingemaanisha kwamba, mamake Mama wa Taifa Margaret Kenyatta ni Mjamaika.

Duru zilisema kile ambacho Rais alinuia kusema ni kwamba, mama mzazi wa mke wa kakake ni Mjamaika.

Kaka mdogo wa Rais, Bw Muhoho Kenyatta, ni mume wa Bi Erica Kenyatta ambaye mamake, marehemu Norma Kanja, alikuwa na asili ya Jamaika.

Bi Kanja alifariki katika mwaka wa 2017, akazikwa bomani mwake Kitisuru, Nairobi. Alikuwa ni mke wa marehemu Jimmy Kanja, na binti wa marehemu Rupert Forbes na marehemu Loretta Forbes.

Katika ziara yake, Rais Kenyatta na Waziri Mkuu Holness walishuhudia utiaji sahihi kwa makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yanajumuisha ushirikiano katika utalii, spoti, turathi na mashauriano ya kisiasa.

You can share this post!

Iran yaionya vikali Amerika

Huenda serikali iliuzia Wakenya kansa 2008

adminleo