• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
KAULI YA MATUNDURA: Pata mwao wa mchakato wa kubuni na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili

KAULI YA MATUNDURA: Pata mwao wa mchakato wa kubuni na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili

Na BITUGI MATUNDURA

MAKALA yangu ya majuma mawili yaliyopita yaliangazia suala la istilahi ‘mzungumzishi’.

Nilikwisha kuangalia istilahi hiyo iliyobuniwa na Seneta Agnes Zani kinadharia na kiutendaji.

Nimekwisha kudai kwamba neno hilo halifai kutumiwa katika nafasi ya ‘spika’.

Mpaka sasa Kenya haina chombo mahususi cha kiserikali ambacho kinaweza kutwikwa jukumu la kuunda, kusawazisha na kusambaza istilahi na msamiati wa Kiswahili.

Hii ni tofauti na ilivyo nchini Tanzania ambako kuna Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA).

Vile vile, nimekwisha kudai kwamba juhudi za vyombo vya habari na watu binafsi (kama vile Dkt Agnes Zani) wanaojifungata masombo kukibunia Kiswahili istilahi kwa minajili ya matumizi ya nyanja maalumu hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono.

Katika makala ya leo, ninapiga hatua na kutathmini hatari iliyopo Kenya kukosa chombo au asasi maalum ya kuunda au kubuni istilahi, kuzisawazisha istilahi mpya na hatimaye kuzisambaza.

Mchakato wa jumla unaopaswa kufuatwa katika uundaji wa istilahi au msamiati ni kwamba; kwanza, lazima kuwe na haja maalum inayochochea istilahi kuhitajika. Kiswahili kwa mfano kinahitaji kutumiwa katika nyanja maalum kama vile teknolojia ya habari na mawasiliano, bungeni, tiba na mahakamani. Nyanja hizi zinahitaji istilahi maalum. Kwa hiyo, lazima dhana inayohitaji kubuniwa istilahi izuke kwanza.

Pili, baada ya istilahi kubuniwa, inapaswa kujadiliwa na jopo la wataalamu wa leksikoni kubaini iwapo inafaa au haifai. Ikiwa istilahi husika inafaa, chombo au wanajopo wanaohusika huiidhinisha ili ianze kutumiwa rasmi.

Wataalamu au asasi husika inaporidhishwa na istilahi mpya, huichapisha na kusambazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari, taasisi za elimu na kadhalika.

Utekelezaji wa hatua ya usambazaji wa istilahi mpya ndiyo hatua ya mwisho inayonuiwa kuipiga muhuri istilahi hiyo kwamba ndiyo inafaa zaidi.

Utundu wa lugha ni kwamba kamwe wasemaji wake hawawezi kushinikizwa kutumia istilahi ambazo wataalamu wamekwisha zibuni na hata zikaidhinishwa kuwa ndizo zinazofaa kutumiwa.

Mifano ambayo inaweza kushadidia kauli hii ni istilahi ‘televisheni/runinga’ (television), ‘kompyuta/tarakilishi’ (computer), ‘kaunti/gatuzi’ (county), chuo kikuu/ndaki/zutafindaki’ (universiry), ‘utandawazi/utandaridhi/ugolobishaji’ (globalisation) na kadhalika.

Kutokana na jozi za istilahi au maneno haya, ni wazi kwamba kuna zile istilahi au maneno yaliyokubaliwa zaidi miongoni mwa wasemaji wa Kiswahili yanapolinganishwa na mengine.

Wasemaji wa lugha wana usemi mkubwa katika mchakato wauundaji, usawazishaji na usambazaji wa istilahi.

Wao ndio wanaoamua ni istilahi au maneno gani yatumiwe lini, wapi na akina nani – hata pale ambapo wataalamu wamekwisha kubuni istilahi nakuipiga muhuri kwamba ndiyo inayofaa zaidi kutumiwa kuelezea dhana fulani.

Baadhi ya wanaleksikoni tajika katika Kiswahili ni pamoja na Mzee Ahmad Sheikh Nabhany wa Mombasa, Prof Rocha Mzungu Chimerah (Chuo Kikuu cha Pwani) na Prof Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Umilisi wa Kiswahili u katika kuyamudu...

Polisi Mungiki wanavyotesa wananchi

adminleo