HabariSiasa

Kifo cha ajabu cha mhudumu wa Cambridge Analytica jijini Nairobi

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PATRICK LANGAT na CHARLES WASONGA 

KIFO cha raia mmoja wa Romania aliyemfanyia kampeni za kidijitali Rais Uhuru Kenyatta kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2013, kilitoa nafasi kwa Christopher Wylie kujiungana na kampuni ya Uingereza ya Cambridge Analytica, imebainika.

Kampuni hii inatuhumiwa kuingilia uchaguzi mkuu wa Kenya 2017 na ule wa Amerika 2016, kulingana na Wylie mwenye umri wa miaka 28 aliyefichua habari hizo kwa mara ya kwanza.

Ni baada ya kifo cha Dan Muresan, mwanawe aliyekuwa waziri wa Kilimo nchini Romania, Loan Avram Muresan, ambapo Bw Wylie aliajiriwa katika kampuni hiyo ya kukusanya na kuchanganua data.

Kimsingi ni Bw Wylie aliyefichua njama fiche na chafu ya Cambridge Analytica ya kuwashawishi wapiga kura kupitia mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook.

Dan Muresan (kushoto) ambaye Christopher Wylie (kulia) amesema alipatikana amefariki katika hoteli moja jijini Nairobi. Picha/ Hisani

“Sikufahamu hayo wakati ambapo nilijiunga na kampuni hii. Aliyefahamu mengi alikuwa mtangulizi wangu ambaye alikuwa akimfanyia kazi Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwenye uchaguzi wa 2013.

Lakini baadaye alipatikana amefariki chumbani mwake katika hoteli moja jijini Nairobi,” akasema huku akikataa kufichua kuelezea jinsi raia huyo wa Romania alivyofariki.

“Hii ndiyo maana nafasi ya ajira ilipatikana katika Cambridge Analytica. Siwezi nikasema aliuawa. Alifariki chumbani mwake hotelini,” akasema  Bw Wylie.

Alikuwa akizungumza katika hafla iliyothaminiwa kwa pamoja na kampuni ya Byline Investigates ya Uingereza na Front Line Club. Hafla hiyo ilipeperushwa moja kwa moja kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Kabla ya kufichua kuhusu kifo cha mtangulizi wake, Bw Wylie aliambia hafla nyingine kwamba kauli ambazo mkubwa wake hakukubaliana nazo zilizimwa.