• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
SOKA MASHINANI: Athena FC yalenga kupiga hatua zaidi michezoni

SOKA MASHINANI: Athena FC yalenga kupiga hatua zaidi michezoni

Na LAWRENCE ONGARO

ATHENA Youth FC ni timu ya kabumbu ambayo iliasisiswa miaka mitatu iliyopita ili kukuza vipaji vya vijana katika kijiji cha Athena na Thika kwa jumla.

Ingawa hivyo, dhamira kuu ya kuasisiwa kwayo ilikuwa kuwaokoa vijana kutoka kwa matumizi ya mihadarati na unywaji wa pombe haramu.

Kocha wa timu hiyo, Fredrick Mwangi anasema alipoanza kazi hiyo ya kuwaleta vijana pamoja, haikuwa rahisi kwa sababu baadhi ya watu walisema hangefanikiwa kuwaleta vijana hao pamoja.

“Mimi na wenzangu wachache tulilazimika kuwahamasisha vijana hao umuhimu wa kucheza mpira bila kuingilia mambo maovu. Baadaye tulinunua mipira michache na vifaa vingine vya spoti ndipo tukaanza kibarua hicho,” anasema kocha Mwangi.

Anasema tangu wakati huo, vijana wengi wameanza kunufaika pakubwa na uchezaji wa soka huku wakishiriki mechi za kirafiki na kuonyesha weledi wao.

Anadokeza kwamba timu hii yenye makao yake katika kijiji cha Athena, eneobunge la Thika, inapanga kuwasilisha matakwa yao kwa mbunge wao Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina ili aingilie kati akawafadhili kwa kuwapa vifaa muhimu vya michezo.

“Nina imani kubwa tukipewa vifaa hivyo, itakuwa ni mwanzo wa vijana kujiendeleza katika mchezo wa soka. Pia ninataka vijana wengi wajiunge na timu hii,” akasema Mwangi alipohojiwa na Taifa Leo.

Hivi majuzi timu hii iliizaba Sports Villa mabao 2-1.

Baadaye vijana hawa waliigonga Kiandutu Youth kwa mabao 2-0.

Pia hapo nyuma walitoka sare na Angaza Youth kwa kulimana mabao 2-2.

Kwa sasa timu hii inapania kujisajili katika Ligi ya kaunti Ndogo ya Thika tayari kwa msimu ujao wa 2020.

“Kile tunachoshughulikia kwa sasa ni kuona ya kwamba tunatafuta ufadhili wa wafanyabiashara na wahisani popote walipo,” akasema kocha huyo.

Akaongeza: “Hata ikibidi tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunaandaa harambee mwakani ili kupata angalau hela za kujisajili na pia kununua vifaa muhimu vya michezo.”

Timu hii ina wanasoka 20 ambao wanaandaliwa katika uwanja wa shule ya msingi ya Athena.

“Kwa sasa ninapanga kuwaandaa chipukizi hawa kwa mechi za kirafiki ili kuwaweka fiti kila mara. Mazoezi huwa tumepanga kati ya Jumatatu hadi Ijumaa ili ifikapo Jumamosi na Jumapili tuwe tunaweza kushiriki mechi za kirafiki,” akafafanua kocha huyo.

Anasema jambo jingine linaloiweka timu hiyo katika dira nzuri ni nidhamu ya hali ya juu.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vigezo muhimu katika ufunzaji wa...

Lionesses kuwaangusha miamba kwenye raga Afrika Kusini

adminleo