• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Hapa ulafi tu, miaka miwili tangu uchaguzi mkuu

Hapa ulafi tu, miaka miwili tangu uchaguzi mkuu

Na VALENTINE OBARA

MNAMO Agosti 8, 2017, mamilioni ya Wakenya walikosa kulala na kuvumilia baridi kali ya asubuhi na jua kali mchana kutwa upigia kura viongozi wa kisiasa.

Wengi walikuwa na matumaini kwamba uamuzi wao ungewaletea mema maishani, lakini miaka miwili baadaye, kilio kimetanda pembe tofauti za nchi raia wakilia kulemewa na maishga huku viongozi wao wakistarehe.

Tangu wabunge, maseneta, magavana na madiwani walipochaguliwa, kilio kikuu kutoka kwa umma kimehusu ulafi wa viongozi hawa.

Wabunge, maseneta na madiwani wamedhihirisha ulafi wao kwa kujijazia mishahara na marupurupu huku wakishinikiza kuongezwa zaidi.

Kwa upande mwingine, magavana wamelaumiwa kwa ufujaji wa pesa za umma hasa kupitia utoaji wa zabuni kwa njia haramu.

Tukio la punde zaidi ni kuhusu jinsi wabunge 85 wakiandamana na wasaidizi wao walivyoamua kuhudhuria kongamano Amerika, ilhali mataifa mengine yanayoshiriki kongamano hilo hayajatuma wajumbe zaidi ya sita.

Inatarajiwa watatumia mamilioni ya pesa za umma katika ziara hiyo ambayo haisaidii kujenga taifa.

Miezi michache iliyopita, mvutano ulitokea kati ya wabunge na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) baada ya viongozi hao kujilipa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.

Hii ni licha ya kuwa wabunge hupokea mishahara ya karibu Sh1.3 milioni kila mwezi, kando na marupurupu tele ikiwemo ya usafiri, ununuzi wa magari na kuhudhuria vikao vya bunge.

Wao hutetea ulafi huu wakidai ni uchochezi uneolenga kufanya wachukiwe na wananchi ambao hutegemea misaada kutoka kwa mishahara hiyo.

“Zile pesa ambazo mbunge hupata huwa anatakikana asaidie kwa matanga, asaidie wale wagonjwa…nikiwapatia simu yangu muangalie ndani nimepata jumbe nne leo asubuhi. Familia za wawili ambao wamefariki wanataka niwasaidie kusafiri kutoka Nairobi hadi Kisii,” Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Bw Richard Onyonka alisema jana alipohojiwa kwenye kituo cha redio.

Kulingana naye, hali hii itabadilika tu ikiwa kila mwananchi atakapowezeshwa kujitegemea kimaisha.

Katika serikali kadhaa za kaunti, magavana na madiwani wanaendelea kufuja pesa za umma bila huruma huku raia wakikosa huduma bora za kimsingi kama afya, maji usafi na barabara.

Kufikia sasa kuna magavana zaidi ya 10 ambao wanachunguzwa au wameshtakiwa kwa madai ya ufisadi. Miongoni mwao ni Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, Sospeter Ojaamong (Busia), Moses Lenolkulal (Samburu) na Ali Korane (Garissa).

Wengine ambao kaunti zao zinachunguzwa ni Cyprian Awiti (Homa Bay), Mohamud Ali (Marsabit), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Mwangi wa Iria (Murang’a), Charity Ngilu (Kitui), Granton Samboja (Taita Taveta) na Okoth Obado (Migori).

Kando na magavana, Afisi ya Msimamizi wa Bajeti ilifichua mbinu zinazotumiwa na madiwani kujilimbikizia marupurupu kwa njia haramu.

Mbinu hizo zinajumuisha kuandaa mikutano nje ya kaunti, kuweka afisi maeneo ya mbali kutoka wadi wanazosimamia, kuandaa safari tele ng’ambo kwa kisingizio kuwa ni za maendeleo na kutesa magavana hadi watengewe fedha za maendeleo ya wadi kinyume ya sheria.

Ni njama hizi ambazo zimesababisha mvutano kati ya madiwani wa baadhi ya kaunti na magavana wao, kama vile Taita Taveta ambako Bw Samboja amelazimika kuanzisha juhudi za kuvunja utawala wa kaunti hiyo.

Imedaiwa pia kuna kaunti ambako madiwani huhangaisha magavana wanaponyimwa zabuni hata kama hawana uwezo wa kutekeleza miradi ipasavyo.

Kaunti nyingine ambapo ulafi wa madiwani umewahi kutishia kukwamisha shughuli za umma ni Makueni, Mandera, Kisumu, Homa Bay, Mombasa, Nairobi, Murang’a na Siaya.

You can share this post!

Thailand kutumia bangi kutibu kansa

Matumaini Wakenya 300 kulipwa fidia ya Sh440b

adminleo