Makala

'Ziara ya Rais Kenyatta eneo la Mlima Kenya italenga kuzima shaka kuhusu uwezo wake'

August 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ana kila sababu ya kuchukua tahadhari kuhusu hali ambapo ngome yake ya ufuasi katika eneo la Mlima Kenya imeonekana ikianza kumpuuza kisiasa.

Hata hivyo, huenda mambo yakabadilika katika kipindi cha mwezi mmoja ujao ambapo amepangiwa kuzuru eneo hilo katika kile kinaonekana ni kuzima ukaidi huo.

Ingawa kuna wale wazee ambao bado wanamtilia maanani kwa msingi kuwa ni mtoto wa mwanzilishi wa taifa Hayati Mzee Jomo Kenyatta, taswira inayovuma Mlima Kenya ni kuwa hana ushawishi wa kina kwa wengi.

Hisia hizo za kutoridhika na uongozi wake huenda akajipata na upungufu wa wapiga kura wa kushawishi wafuate mradi wake Wa urithi Wa urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2022.

Athari za hali hiyo ni kuwa, huenda ufuasi wake ukipungua ajipate katika hali ngumu ya kukusanya asilimia ya maana ya kura zote za eneo la Mlima Kenya kumwezesha kuchangia matokeo ya uchaguzi huo huku kukiwa na kambi mbili za ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ katika ngome hiyo.

Aidha, huenda cheche hizo za upinzani zikatoa mazingira mwafaka kwa mahasidi wake wa kisiasa kupenya ngome hiyo na kuwarai wenyeji wajiunge na mirengo yao, hali ambayo itamkanganya Bw Kenyatta kisiasa. Upinzani huo unaegemea kutoridhika na masuala ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima Wadogowadogo kanda ya Mlima Kenya Bw Erastus Muriuki, serikali ya Bw Kenyatta imelemewa kabisa kudhibiti kudorora kwa riziki katika safu ya kilimo.

“Ukilinganisha hali ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wake, Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki, hali imekuwa si hali tena na kuna kilio kikuu miongoni mwa jamii ya wakulima. Hali hiyo imempunguzia Bw Kenyatta uungwaji mkono wa dhati,” akasema Bw Muriuki.

Bw Muriuki alisema kuwa bei za bidhaa za kilimo zimesambaratika huku mfumo wa utozaji ushuru ukipanda na hatimaye kumwacha mkulima akiwa hana lake.

“Wakati wa Bw Kibaki bei ya maziwa kwa lita moja yakinunuliwa kutoka kwa mkulima ilipanda hadi Sh45. Kwa sasa, bei hiyo imeteremka hadi Sh28. Bidhaa za uzalishaji zilikuwa hazitozwi ushuru wa VAT lakini Bw Kenyatta ameleta ushuru huo kwa kiwango cha asilimia 16. Ukizingatia hayo, mzalishaji maziwa anatamauka,” akasema.

Aidha, Bw Muriuki aliteta sekta zingine muhimu kama za majanichai, kahawa na pia mboga na matunda ziko katika hali isiyofurahisha; hasa kwa wakulima.

 

“Hivi karibuni tumepata visa ambapo bonasi za majanichai zimepunguka au kupotea. Bei ya kahawa imeanguka huku soko likiyumbishwa na madalali matapeli,” akasema.

Suala lingine ambalo linatishia umaarufu wa Bw Kenyatta katika ngome yake ni kuchipuka upya kwa genge fidhuli la Mungiki.

Kundi hilo limeripotiwa kuzindua upya harakati zake za kutoza ushuru haramu sekta ya usafiri wa umma na ile ya ujenzi wa nyumba.

Genge hilo limeripotiwa kushiriki mauaji ya kiholela katika Kaunti za Kajiado, Kirinyaga, Murang’a na pia Nakuru na maafisa wa usalama wanaonekana wazi kutokuwa na uungwaji mkono wa kisiasa kulikabili.
Nao wamilki wa magari ya usafiri wa umma wanalalama kuwa utawala wa Rais Kenyatta unawalenga kwa sera kandamizi za uagizaji magari ya kubeba abiria 14.

Muungano huo ulisema kwa sasa Waziri wa Uchukuzi, James Macharia amezima kuagizwa kwa magari hayo licha ya kupewa hakikisho na serikali kuwa marufuku hayo hayatatekelezwa.

Naibu mwenyekiti wa muungano huo Bw Steve Murunga alisema wakati wa mahojiano kuwa serikali ilikuwa imetoa idhini ya kuagizwa kwa magari hayo 2,000 hadi mwaka 2018 lakini baadaye Bw Macharia akapinga kutoa idhini nyingine.

“Hii ni licha ya kuwa, Rais alipokuwa Waziri wa Fedha na pia Naibu Waziri Mkuu katika utawala wa Kibaki alisema kuwa magari hayo hayatazimwa kwa kuwa yanahami vijana wengi kujitafutia riziki. Hata hivyo, akiwa mamlakani – wakati tunatarajia kuwa atahakikisha kuwa magari hayo hayafutiliwi mbali – yanazimwa,” akasema Bw Murunga.

Murunga alisema ikiwa marufuku hayo yatadumishwa, basi yatanyima vijana 500,000 nafasi za kazi.

Mwenyekiti wa Wamilki Magari ya Usafiri wa Umma eneo la Mlima Kenya, Bw Micah Kariuki anasema marufuku hayo yatalenga eneo (ngome) ya Rais Kenyatta kwa kuwa “wao humilki asilimia 80 ya magari yote yanayohudumu hapa nchini.”

Mwingine anayeteta kuhusu marufuku hayo ni mwenyekiti wa chama cha matatu cha 4NTE Bw Wilfred Kimotho anayesema hatua hiyo ni kinyume na sera ya serikali ya Kenyatta ya kuunda nafasi za kazi hapa nchini.

Aidha, anateta kuwa wawekezaji wa kiwango cha chini katika sekta ya uchukuzi  ndio watakaoumia zaidi kwa kuwa hawawezi kumudu gharama ya mabasi.

Suala la ufisadi nalo limeibuka kama kishawishi kingine cha kumpunguzia kiongozi wa nchi umaarufu wake.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe hivi majuzi aliteta kuwa kuna ufisadi wa viwango vya juu katika afisi za maeneobunge ambapo wenyeji wanapotuma maombi ya kupewa mikopo ya hazina za maendeleo mashinani wanahangaishwa.

“Hali hiyo haiwatatizi wenyeji pekee mbali inahujumu umaarufu wa Rais Kenyatta. Visa hivyo visipothibitiwa, tutajipata tuko na kazi ngumu ya kuwaeezea wenyeji kuwa serikali yao iko na uwazi na maadili,” akateta Bi Kibe.

Katika nyanja nyingine, aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Bw Kabando wa Kabando tayari ameelezea hisia zake kuhusu ufisadi wa Anglo-Leasing ambapo licha ya wafuasi wa serikali ya Kenyatta kushikilia kuwa sakata ya Anglo-Leasing isinufaike na malipo ya Sh1.4 billioni, Bw Kenyatta aliishia kukiuka msimamo wao na akaamrisha zilipwe.

Bw Kabando anateta kuwa wabunge walikuwa wakitumiwa visivyo kwa kushinikizwa wapige muhuri  ufisadi kwa kuidhinisha malipo hayo.

Hali hiyo inaonekana kushika kasi kila kuchao kwa kuwa hivi majuzi Baraza la Wazee la Jamii ya Agikuyu lilionya kuwa litaongoza wafuasi wao kujiondoa kutoka chama cha Jubilee ikiwa Rais hataidhinisha chama hicho kiimarishwe.

Mtindo

Aidha, baraza hilo lilisema kumejitokeza mtindo wa maafisa wa chama hicho wa kuwaacha viongozi wake walio matatani bila ya kuwatetea na kuwaunga mkono.

Katika mkutano uliofanyika katika Mkahawa wa Homeland Kaunti ya Kiambu, wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw Wachira Kiago walisema chama cha Jubilee kinafifia na hakina uwezo wa kushindana na upinzani iwapo uchaguzi utaandaliwa leo hii.

Alisema kwa sasa chama hicho kimesambaratika kiasi cha kutofahamika na wasajili wapya huku akisema uongozi wa sasa wa chama hicho haufai yeyote aliye na nia ya kuimarisha ushindani wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema hali hiyo imezua utundu miongoni mwa viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya Jubilee huku baadhi yao wakijihusisha na mirengo tofauti katika siasa za leo.

“Tuko na wabunge na madiwani waliohamia mirengo mingine na utawapata wakiandamana na vinara wa vyama vingine katika muungano wa Jubilee badala ya kuimarisha chama chao. Hali hiyo imesababishwa na ukosefu wa uongozi ndani ya chama tawala,” akateta.

Bw Kiago alisema msimamo wa baraza hilo ni kuunga mkono viongozi wote wanaohudumu chini ya Rais Kenyatta akiteta kuwa baadhi ya wabunge wa Jubilee ndio wanaoandaa miswada ya kuwang’atua mamlakani mawaziri wa serikali wakishirikiana na upinzani.

Hali ikianza kujiunda kwa misingi hiyo, ni taharuki ya kila mwanasiasa aliye na nia ya kuendelea kuchaguliwa na ikiwa Rais Kenyatta hatachukua tahadhari na kubadilisha hali, basi merikebu yake ya kisiasa itazama huku yeye mwenyewe akiwa ndani.