Makala

BONGO LA BIASHARA: Sura mpya ya uchoraji na jinsi vijana wanavyofaidi

August 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MAOSI

SANAA ya uchoraji katika jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kupata taswira mpya, kutokana na idadi kubwa ya vijana wenye vipaji wanaoendelea kujitosa ulingoni ili kujichumia riziki.

Licha ya kero ya ukosefu wa ajira, vijana wanaweza kubuni mbinu mbadala ya kujipatia hela badala ya kusubiri kazi ya kuajiriwa, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa baadhi yao.

Kinyume na awali ambapo watu wengi walichukulia kuwa kazi ya uchoraji ni mali ya makavazi au vituo maalum vya maonyesho, hali imebadilika kwani watu wengi wameajiriwa katika sekta ya kuchora.

Vijana wengi sasa wanaweza kupitisha ujumbe muhimu kwa jamii yao kupitia sanaa ya uchoraji, ambapo wanatumia ustadi wa kuibua michoro inayovutia hisia za watu.

Aidha, kwa mtaji mdogo wamefanikiwa kustawisha karakana zao ndogo mijini na vijijini, zinazotoa mafunzo ya uchoraji, kupaka rangi, uchongaji vinyago na maonyesho ya kazi za sanaa kwa umma.

Akilimali ilipotaka kubaini ni wapi hasa mchoraji hupata hamasa yake, Oscar Muigai alikuwa na jibu kamili kwani alisema ni mambo ya kawaida yanayomzunguka binadamu ndiyo humpatia msukumo.

Oscar Muigai anasema kuwa ni mwasisi wa kundi la vijana sita kutoka mjini Nakuru na kaunti ndogo za Molo na Rongai, waliojiajiri katika tasnia ya kuchora ndiposa wanajitegemea

Kulingana na Muigai, michoro yake ni ya aina mbalimbali, mara nyingi amejikita katika uchoraji wa kubuni kwa kudadisi hali halisi ya watu na jinsi wanavyokabiliana na changamoto za kila siku.

“Watu wengi wanapenda kujihusisha na michoro ya kutia moyo, hasa ile inayohusu hali zao za maisha bila kujali bei yake,” aliongezea.

Muigai anasema anajaribu kadri ya uwezo wake kuchanganya mtindo wa kisasa na zamani ili kuyafikia makundi yote ya watu, kwani kazi ya uchoraji ni kama fasihi na mara nyingi hili ni zao la jamii.

Kazi hii anayoifanya na vijana wenzake katikati ya mji wa Nakuru inapendwa na watu wengi wanaofika katika karakana yao inayopatikana Section 58 kujitazamia urembo wa michoro.

Wakati wa mchana kundi fulani hufanya kazi ya kuchora na wengine kutafuta wateja. Hata hivyo, wakati mwingine utakuta mahitaji ya soko ni mengi kuliko kiasi cha kazi wanazochora.

“Mnamo 2015 hatukuwa na sehemu maalum ya kuhifadhi bidhaa zetu, ila tuliweka akiba ya kukodisha chumba cha kuweka michoro yetu ili kuhakikisha iko salama,” Muigai akasema.

Wateja

Msanii huyu aliongezea kuwa wanunuzi wake wengi ni wasanii na wanamitindo wanaopania kutangaza bidhaa zao kwa njia rahisi na nafuu ambayo mtu wa kawaida anaweza kumudu.

Anaungama kupitia sanaa mfanyabiashara anaweza kutangaza bidhaa zake kwa Sh5,000, muradi afahamu soko na mahitaji ya wanunuzi, akiamini kuwa bado kuna ushindani mkali kutoka kwenye majarida na runinga.

Mara nyingine katika tamasha za haiba anatumia mtindo wa kupuliza rangi ukutani, mara nyingi ukifahamika kama graffiti inayopendwa na kuenziwa na waimbaji wa miziki ya kufokafoka.

Muigai anasema alianza kuchora tangu akiwa katika shule ya msingi, lakini zaidi ni bidii za mtu zinazoweza kumfikisha mbali. Kiu ya kujifunza kitu kipya kila wakati ikiwa kiungo muhimu cha kumpatia mtu msukumo wa kila siku kujiboresha.

Tangu ajiunge na shule ya upili amekuwa akijitegemea kutekeleza kila kitu, kama vile kulipa kodi na kujinunulia kipande cha ardhi ambapo ameanzisha kilimo, ndiposa akaamua kufanya sanaa ya uchoraji kuwa kama kazi.

“Kazi ya kuchora ni kama kazi ya ofisini inayoweza kumpatia mtu hela ndefu mradi mchoraji apige msasa ujuzi wake na kuipenda kazi ya mikono yake,” aliongezea.

Asema mchoro mmoja huuzwa kati ya 2500-4500, isipokuwa ile ya watu maarufu kama vile viongozi ambayo inaweza kuzidi 10,000.