• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:11 PM
AKILIMALI: Kilimomseto kinavyowafaa marafiki watatu

AKILIMALI: Kilimomseto kinavyowafaa marafiki watatu

Na CHRIS ADUNGO

MARAFIKI watatu, Esther Muthoni, Beth Wangare na Sophia Moochi walijitosa katika ulingo wa ukulima, na hasa upanzi wa mboga za kiasili za kila sampuli zikiwemo mchicha, sukumawiki, dania, mnavu, vitunguu na ‘terere’ ili kuwavuta wateja zaidi wa mazao haya kwa wakati mmoja.

Kwa mtaji mdogo mno mnamo 2015, walianza kwa kupanda mchicha pekee katika magunia na idadi ya wateja ilipozidi kuongezeka, ndipo waligeuza kilimo chao ili kufikia kiwango kikubwa cha wanunuzi waliozidi kumiminika kitaluni pao wakitaka kuuziwa mboga za kienyeji.

Ingawa hivyo, wanashauri kwamba desturi ya upandaji mimea kimseto (Mixed Farming) ni mojawapo ya njia zenye kuhimiza utumiaji bora wa shamba pamoja na udhibiti wa wadudu wa aina tofauti (viruka-majani, viwazi, mende-jani, kichimbabua na kadhalika.

Mixed Farming inayoendeshwa kwa sasa na marafiki hawa watatu wa kufa kuzikana, ilichochewa na udogo wa kipande cha shamba la takribani nusu ekari walilolikodi mwishoni wa 2016 ili kuanzisha upanzi wa mchicha pamoja na mimea mingine waliyomudu kupanda.

Mkopo wa kundi la akina mama uliwapiga jeki hasa katika juhudi za kulipa ada ya Sh5,000 za kukodi shamba hilo.

Kwa sababu waliendesha kilimo katika eneo la chemichemi, walihitajika kuchimba mitaro iliyogeuza mikondo ya maji nje ya shamba na kwa wakati huo ikiondosha maji yaliyotapakaa shambani wakati ambapo hayakuhitajika kwani yangenyima mimea hewa safi. Walijaribu kulainisha udongo mweusi aina ya ‘clay’ unaopasukapasuka sana kisha wakapunguza tindikali shambani kwa kufanyia ‘liming’.

Hatua ya awali ilihitaji mbolea ya mchanganyiko wa samadi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Baadaye, ardhi tambarare ilipatiwa muda wa kutosha ili kurejesha uwezo wake wa kuhimili mimea ya kila aina.

Wakinunua mbegu zilizofanyiwa ukaguzi katika Chuo Kikuu cha Egerton (Egerton Seed Unit), Esther, Beth na Sophia walipata nasaha ya bure kuhusu teknolojia ya kilimo. Isitoshe, walifanyiwa tathmini ya mchanga katika shamba lao bila ada yoyote.

Eneo la Ol Kalou likiwa na baridi kali na mvua nyingi, wakulima hawa wanaeleza kwamba changamoto yao kubwa zaidi ni ya udongo kushikilia maji kwa wingi (waterlogging).

Hali hii hunyima mimea hewa ya kutosha wakati inapohitaji kukua na kutanua zaidi majani. Isitoshe, baridi kali huweza kuchochea matawi yaweze kukunjana ovyo na kupoteza rangi ya kijani kibichi kwenye ncha za majani. Majani haya baadaye hugeuka rangi na kuanza kuwa ya samawati au manjano.

Walipohakikisha kwamba wamekabili hali hizi zote vilivyo, walipanda mchicha na vitunguu maji katika hatua ya mwanzo ya kufanyia shamba lao majaribio.

 

Wakulima Esther Muthoni, Beth Wangare na Sophia Moochi wapalilia mboga wanazozipanda kwa mseto katika shamba wanalolimiliki kwa pamoja katika Kaunti ya Nakuru. Picha/ Chris Adungo

Mimea yao ilipofana na kunawiri zaidi, waliongeza mboga za terere pembeni na kupatia shamba lao muda wa miezi miwili zaidi kabla ya kuvuna mazao yao ya kwanza. Kipato kutokana na mchanganyiko wa mboga hizi ni kizuri, majani yakaanza kuwa manono zaidi.

Majani manne ya mchicha yalianza kuuzwa kwa Sh10 huku kila eneo la sentimita 100 kwa 100 mraba likiwa na uwezo wa kutoa mmea wenye majani kati ya 800 na 1,000.

Kwa kiwango cha nusu ekari ya shamba, haya ni majani mengi sana.

Wakulima wengi katika eneo hilo wameendelea kiteknolojia kiasi cha kulazimika kutumia kiwango kidogo cha maji kutokana na paipu zilizopita ardhini na vishimo katika sehemu inayokutana na mmea, hasa katika nyakati za kiangazi.

Unyunyiziaji maji kwa paipu au chupa almaarufu ‘Drip Irrigation’ ni maarufu sana miongoni mwa wakulima hawa watatu ijapokuwa wanakiri kwamba ni ghali sana kudumisha mbinu yenyewe hasa kipande cha shamba kinapoongezeka na mseto wa mmea kupanuka.

Matokeo yake yatamfaidi mkulima kila wakati na paipu zinaweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu. Ikilazimu, jenereta husukuma maji kutoka mtoni, maji yanapopungua na kuunganisha na mikondo hii ya maji inayoyahifadhi.

Mbali na kufanya unyunyiziaji wa kibinafsi, almradi mimea ipo shambani, huwa inanyonya maji kupitia mizizi yake polepole na taratibu. Terere zikiaminika kuongeza kiwango cha damu mwilini, pia huponya maradhi ya vidonda vya tumbo.

Zikiwa miongoni mwa mboga maarufu sana za kienyeji, Esther, Beth na Sophia hawana budi kuwabainishia wanunuzi kwamba teknolojia ya kisasa imefanikisha upanzi na ukuzaji wa mboga hizi za kiasili zinazochukua muda mfupi kukomaa mbali na kuhitaji kiwango kidogo cha uangalizi.

You can share this post!

BIASHARA MASHINANI: Kilimo cha sukumawiki na nyanya chamfaa...

Manchester United yamezea mate Eriksen wa Spurs, Arsenal...

adminleo