• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Serikali kuendesha operesheni kali ya usalama katika kaunti 6

Serikali kuendesha operesheni kali ya usalama katika kaunti 6

Na BARNABAS BII

KAMISHNA wa Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya amesema kuwa serikali inapanga kaunzisha operesheni kali ya kukabiliana na wahalifu katika kaunti sita zilizokumbwa na ukosefu wa usalama.

Bw Natembeya alisema kuwa maafisa wa usalama pia watarejesha bunduki zinazomilikiwa kiharamu wakati wa operesheni hiyo.

Kamishna alifichua hayo baadaya kukutana na maafisa wa ngazi ya juu wa usalama kutoka Kaunti za Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Samburu, Elgeyo Marakwet na Laikipia mjini Eldoret.

“Tumeamua kuwa maafisa wa usalama watashirikiana na wenyeji kuwasaka wahalifu wanaotatiza usalama katika kaunti hizo,” akasema Bw Natembeya.

“Tayari tuna orodha ya viongozi wa wahalifu hao na sasa tutawaandama mmoja baada ya mwingine hadi pale tutaangamiza uhalifu,” akaongezea.

Polisi wa Akiba (KPR) pia watahusishwa katika operesheni hiyo.

Alionya kuwa wanasiasa na watu watakaotatiza operesheni hiyo watakamatwa na kufikishwa kortini.

“Wizi wa mifugo na mashambulio mengineyo yanarudisha nyuma maendeleo katika ukanda huu . Wanasiasa wanaotatiza juhudi za kuleta amani watakamatwa,” akasema.

You can share this post!

MBIYU KOINANGE: Mwanasiasa aliyetuliza hasira za Mzee...

Kitui yafaulu kushona sare za machifu wote nchini

adminleo