Habari Mseto

'Akaunti za kampuni katika kesi ya Kimwarer na Arror zifungwe'

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

AKAUNTI za kampuni mbili zilizohusika katika kashfa ya mabwawa ya Kimwarer na Arror zimefungwa.

Hakimu Mkazi, Bi Caroline Muthoni aliamuru akaunti za Stanlib Wealth Amannah Properties Limited na Azepco General Trading Company, zilizoko katika benki ya Standard Chartered zifungwe kwa muda wa siku 180 polisi wakamilishe uchunguzi.

Bi Muthoni alimruhusu afisa anayechunguza kesi hiyo Isaac Ogutu atwae nakala za akaunti hiyo kubaini pesa zilizopitishwa mle kati ya Desemba 2019 hadi sasa.

Mahakama iliamuru taarifa za ushahidi zinakiliwe kutoka kwa maafisa wakuu katika benki hiyo.

“Baada ya kupokea ushahidi wa Bw Ogutu hii mahakama inakubaliana naye kwamba uchunguzi unapaswa kufanywa kuhusu kampuni hizi za Italia,” Bi Muthoni alisema.

Akitoa uamuzi, hakimu alimruhusu Bw Ogutu apige darubini akaunti hizo.

Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Bi Muthoni katika mahakama ya Milimani, Bw Ogutu alisema polisi wamepashwa habari kwamba kampuni ya Stanlib ilikuwa imepanga kutoa Sh734.5milioni kutoka kwa akaunti yake iliyoko tawi la Standard Chartered, Sarit Centre.

Stanlib ilikuwa ikiipa kampuni ya Azepco kitita hicho. Azepco iko na akaunti Dubai.

Bw Ogutu aliambia korti Stanlib ilihusika na ujenzi wa bwawa la Kimwarer ilhali Azepco ilihusika na ujenzi wa bwawa la Arror.

Korti ilijulishwa kuwa Azepco ilipokea Sh672 milioni kutoka kwa kampuni ya Italia inayofahamika kama CMC De Rave inayodaiwa ilihusika mno na bwawa la Arror.

Hakimu alifahamishwa benki ilipewa nakala za ombi hilo lililowasilishwa kortini.

“Ni heri akaunti hizi zifungwe ukweli ujulikane,” alisema Bw Ogutu.

Pia alisema anataka kuchunguza kiasi cha pesa kilichowekwa na kutolewa katika akaunti.

Mahakama ilifahamishwa serikali ilipoteza zaidi ya Sh63bilioni katika miradi hiyo.

Bi Muthoni alielezwa Bw Ogutu alifika katika afisi za Stanlib na kumpata meneja mkurugenzi, Bw Christopher Michael Mwebesh na afisa mwingine, Bi Evalyn Kinyua, waliomweleza kuwa benki ya Standard Chartered iliwafahamisha kuhusu ombi la kufungwa kwa akaunti zake.