• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Komeni kutegemea misaada na kuwa walafi, Amerika yaikemea Kenya

Komeni kutegemea misaada na kuwa walafi, Amerika yaikemea Kenya

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI ya Marekani imeikemea Kenya kwa kuendelea kutegemea misaada kutoka nje, ilhali haijachukua hatua za kutosha kumaliza ufisadi.

Balozi wa nchi hiyo hapa Kenya, Bw Kyle McCarter, alisema Alhamisi kwamba Kenya imeshindwa kukabiliana na wizi wa pesa za umma, na akahimiza vyombo vya habari viwe mstari wa mbele kuangazia maovu hayo.

Alikuwa akizungumza katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi, alipofungua rasmi kongamano la kila mwaka la Vyombo vya Habari.

“Naomba nizungumze kama mwanasiasa, kwa kuwa nimekuwa seneta kule Marekani kwa miaka mingi. Kenya ni nchi inayoweza kuendelea kiuchumi kama si huu wizi wa pesa za umma,” akasema.

Bw McCarter alishangazwa na jinsi ambavyo serikali imekuwa ikiendelea kukopa na hata kutegemea misaada ya kigeni, ambayo inapoingia tu, huishia mikononi mwa watu wachache walafi.

“Hapa Kenya mna bahati sana kwamba mbali na raslimali iliyopo, mna nguvukazi ya vijana wenye nguvu na uwezo wa kutimiza maendeleo makubwa. Kwa bahati mbaya hakuna linaloendelea na mumesalia kutegemea misaada kutoka kwa wahisani,” akaeleza.

Balozi huyo alivihimiza vyombo vya habari vichukue msimamo na kuangazia uongozi mbaya, akisema ni kupitia kumulikwa kwa mambo hayo ambapo nchi inaweza kujikwamua kutoka uozo unaowanufaisha watu wachache.

“Nataka niseme wazi kuwa Marekani na hata Canada, tupo hapa kusimama na wanahabari watakaohangaishwa kwa sababu ya kusema ukweli kuhusu yanayoendelea. Ni ukweli pekee ambao utawafanya viongozi na wasimamizi wengine wa raslimali kugutuka na kutenda linalostahili,” akasema.

Kongamano la mwaka huu la vyombo vya habari linaangazia mada ya Demokrasia na Uwajibikaji Serikalini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Habari ya Nation (NMG), Bw Stephen Gitagama, aliendeleza hoja ya uwajibikaji wa vyombo vya habari na kuhimiza kuwa wanahabari waangazie masuala ya jamii kwa njia ya haki bila kuogopa.

“Wajibu wa magazeti ni kumdhalilisha anayetesa wanyonge, na kumpa nguvu anayekandamizwa. Jukumu hili, hatuwezi kuliepuka kama wanahabari,” akasema Bw Gitagama.

You can share this post!

Sh100m: Wabunge wa Kenya ndio wengi zaidi duniani kwa...

Amerika si salama tena, ulimwengu waonywa

adminleo