Michezo

Arsenal yaziba nyuma EPL iking'oa nanga leo usiku

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA na MWANGI MUIRURI

HUKU dirisha la uhamisho Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) likiteremsha pazia, klabu ya Arsenal imejipa vifaa vya kujikinga kutokana na mipigo ya uvamizi wa wapinzani ugani.

Vilevile, msimu mpya wa EPL unaanza rasmi leo Ijumaa usiku wakati Liverpool itavaana na Norwich City mwendo wa saa nne usiku (saa za Afrika Mashariki).

Vifaa hivyo vipya vya meneja Unai Emery ndani ya uga wa Emirates ni nguli David Luiz kutoka Chelsea pamoja na Kieran Tierney, 22, kutoka Celtic. Hawa wana dhamana kubwa kuhakikisha Arsenal haivuji na wafuasi wa Arsenal wanaamini huenda msimu huu wakaepuke kinaya cha kuwa katika mduara wa tano bora katika jedwali lakini katikati mwa jedwali ilo hilo katika usajali wa kutikisiwa nyavu zake.

Hali hii imetokana na kuhama kwa tegemeo Laurent Kosielny ambaye amerejea nyumbani Ufaransa kuwajibikia timu ya Bordeaux huku pia umri ukiwa umesonga akiwa katika mduara wa miongo mitatu sasa ya uhai wake.

Luiz, raia wa Brazil ana umri wa miaka 32 na alikuwa ametia mkataba wa miaka miwili ugani Stamford Bridge Mei lakini ameamua kujiunga na wanabunduki hao ghafla.

Eddie Nketiah ambaye ni chipukizi wa Arsenal aliazimwa timu ya Leeds United kwa msimu mmoja na ambapo anatarajiwa kujiimarisha kimakali kwa kuwajibikia timu ya kwanza. Leeds imekopa huduma zake.

Habari za kushangaza kwa mashabiki hao wa Arsenal ni kuwa kiungo mshambulizi Alex Iwobi na ambaye ni raia wa Nigeria amehamia timu pinzani ya Everton kwa kandarasi ya miaka mitano, hali ambayo sasa inaonekana kwa kuashiriwa kuwa timu hii ya Everton itakuwa moto wa kuotea mbali msimu huu wa 2019/20.

Everton imejiimarisha kwa kusajili vifaa vingine kama Jonas Lossl, Djibril Sidibe, Andre Gomes, Fabian Delph, Philippe Gbamin na Moise Kean.

Manchester City wakiwa mabingwa watetezi wamejipa huduma za Pedro Porro kutoka Girona huku Andy Carroll akirejea katika timu yake ya zamani ya Newcastle naye ‘kifaru’ mshambuliaji wa Manchester United, Romelu Lukaku akijiunga na Inter Milan, miongoni mwa habari nyingine nyingi kuhusu uhamisho huo.

Hata hivyo, kuna fursa za kuuza vifaa kwingineko katika soko pana la Ulaya ambapo madirisha mengine yatakuwa wazi hadi Septemba 2, 2019.