Wahitimu wa MKU wahimizwa kutumia elimu kiubunifu zaidi
Na LAWRENCE ONGARO
WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) wamehimizwa Ijumaa kujiamini na shahada walizopokea na kubuni ajira zao wenyewe.
Mwenyekiti wa bodi ya MKU Profesa Simon Gicharu amewataka wahitimu hao wawe mstari wa mbele kuonyesha ujuzi wao katika ushindani mkali uliopo katika sekta ya ajira.
Zaidi ya wahitimu wapatao 6,666 wamefuzu katika masomo tofauti katika chuo hicho eneo la Happy Valley, Landless, mjini Thika.
Wakati wa hafla hiyo viongozi kadha walikuwa miongoni mwa wahitimu hao.
Baadhi yao ni aliyekuwa mbunge wa Molo Bw Joseph Kiuna, mbunge wa Kasipul Kabondo Bw Charles Obondo Were, na mbunge wa Igembe Kusini Bw John Murigi.
Prof Gicharu amesema Chuo cha Mount Kenya kimetenga Sh5 milioni zitakazotumika kufadhili wanafunzi kusafiri nchi za nje kwa masomo ya juu.
Pia chuo kitafanya juhudi kujenga vyumba 3,000 vya wanafunzi kwa gharama ya Sh2.5 bilioni eneo la Happy Valley mjini Thika.
Amewahimiza wanafunzi kutegemea jasho lao bila kutafuta mikato kupata utajiri.
“Ni vyema kujitegemea na kufanya bidii ili kupiga hatua zaidi. Lakini tabia ya kutegemea njia za mkato haiwezi kunufaisha mtu,” amesema Prof Gicharu.
Alisema MKU imefanya juhudi na kufungua kituo cha runinga cha TV 47 Channel ambacho kimeajiri watu kadha.
Utafiti na ubunifu
Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa Stanley Waudo amesema kinazingatia sana maswala ya utafiti ma ubunifu.
“Ningetaka kuwahimiza muwe wabunifu mtakapokuwa huko nje. Maisha ni magumu na kwa hivyo ujuzi wako ndiyo itakuwa ngao yako,” amesema Prof Waudo.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Chansela wa chuo hicho, Prof John Struther na wageni wengine wakiwemo Prof Richard Macharia kutoka Chuo cha London na Dkt David Mully ambaye ni mwanzilishi wa Mully Children’s Family.
Wahitimu wapatao 337 wamepata shahada za uzamili halafu wawili wakapata shahada za uzamifu.