Kimetto kuwania ubingwa Vienna City Marathon
Na GEOFFREY ANENE
BAADA ya kuthibitisha Machi 8 kwamba hatashiriki mbio za Boston Marathon nchini Marekani hapo Aprili 16, mshikilizi wa rekodi ya dunia Dennis Kimetto sasa ameingia mbio za Vienna City Marathon zitakazofanyika nchini Austria mnamo Aprili 22, 2018.
Kimetto, 34, ambaye aliweka rekodi ya dunia ya saa 2:02:57 aliposhinda mbio hizi za kilomita 42 jijini Berlin nchini Ujerumani mwaka 2014, atakuwa mshikilizi wa kwanza kabisa wa rekodi ya dunia ya marathon kuwahi kushiriki Vienna City Marathon katika kipindi cha miaka 34.
Mkenya huyu, ambaye umaarufu wangu umepungua sana tangu ushindi huo wa Berlin, analenga kutumia Vienna City Marathon kufufua taaluma yake.
“Nimefaulu kufanya mazoezi kwa muda mzuri bila jeraha,” Kimetto ameambia Shirikisho la Riadha duniani (IAAF) katika mahojiano Jumatano.
Marathon ya mwisho ambayo Kimetto alimaliza ni London Marathon nchini Uingereza mwaka 2016 aliporidhika na nafasi ya tisa kwa saa 2:11:44. “Naamini nina uwezo na ninataka kuonyeshana ubabe wangu jijini Vienna.
“Ikiwa hali itakuwa nzuri, basi nitajaribu kuvunja rekodi ya Vienna City Marathon ya saa 2:05:41, ambayo iliwekwa na Muethiopia Getu Feleke mwaka 2014.
“Cha muhimu ni kwamba baada ya msururu wa matokeo duni katika mbio, nitatafuta kumaliza marathon kwa muda mzuri tena.”