TAHARIRI: Tuzishangilie Gor, Bandari katika CAF
Na MHARIRI
LEO Jumamosi Bandari inaanza safari ya kupiga hatua katika kandanda ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) maarufu kama Confederation Cup itakapoalika Al Ahli Shandy ya Sudan katika uwanja wa Kasarani, Nairobi.
Nao mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia wanazuru Burundi kesho Jumapili kukabiliana na Aigle Noir kwa mechi ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).
Hiyo ni fursa nzuri, kwa mara nyingine, kwa klabu za Kenya kutangaza ubabe wa taifa hili katika mchezo huo, unaopendwa zaidi duniani, hapa barani Afrika.
Aghalabu klabu za Kenya zimekuwa zikisuasua zinapofika kwenye midani ya kimataifa maadamu nyingi hutolewa katika hatua za mwanzo mwanzo.
Ni mwaka 2018 tu ambapo Gor ilijizatiti na kufika hatua ya robo fainali kabla ya kuondolewa na RS Berkane ya Morocco kwa kuangushiwa kichapo kizito.
Bila kuzingatia ufanifu wa K’Ogalo kwenye michezo ya Cup Winners Cup ya Afrika mnamo 1987 ilipopiga Esperance ya Tunisia na kutwaa ubingwa wa bara, Gor, sawa na klabu nyinginezo maarufu nchini mathalan AFC Leopards, Tusker, Bandari, Mathare United, Ulinzi na Sofapaka, imekuwa ikipata matokeo yasiyoridhisha kamwe.
Mojawapo ya sababu ambazo hutolewa kwa kudorora kwa timu hizi ni kwamba ufadhili wa klabu za taifa hili zinazocheza soka ya kimataifa huwa mdogo mno usioziwezesha kupiga hatua ya maana.
Kwa sababu hiyo, imewahi kuripotiwa kuwa baadhi ya klabu, kutokana na ugumu huo, huamua ‘kuuza’ mechi kwa kuruhusu kufungwa kwa urahisi ili ziondokane na masumbuko hayo.
Athari za tatizo la kifedha
Ingawa tatizo la kifedha huathiri klabu vibaya, uzalendo unahimiza timu kujizatiti zinapofuzu kuwakilisha taifa katika mashindano ya hadhi kama hii. Ni ombi letu kuwa mara hii klabu hizi mbili, Gor na Bandari zitafadhaliwa vya kutosha ili kushiriki fainali hizi kwa motisha na ari ya hali ya juu.
Hata hivyo, kipo kiungo muhimu kinachoweza kufidia ukosefu wa fedha za kutosha; mashabiki wamiminike kwa wingi uwanjani ili kuwatia ghera wanasoka wa timu hizi zinapochuana na majabali wa bara kuanzia leo.
Hatufai kutegemea mashabiki wanaotoka Mombasa hadi Nairobi, kila mpenda soka ajitolee kwa hali na mali kuipa moyo Bandari leo.